Mose Na Kichaka Kinachowaka Moto
1 Basi Mose alikuwa anachunga mifugo ya Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani. Mose akapeleka mifugo mbali nyuma ya jangwa, naye akafika Horebu, mlima wa Mungu. 2 Huko malaika wa Bwana akamtokea Mose katika mwali wa moto kutoka kichakani. Mose akaona kwamba ingawa kile kichaka kilikuwa kinawaka moto, kilikuwa hakiteketei. 3 Ndipo Mose akawaza, "Nitageuka sasa nione kitu hiki cha ajabu, nami nione ni kwa nini kichaka hiki hakiteketei."
4 Bwana alipoona kuwa amegeuka ili aone, Mungu akamwita kutoka ndani ya kile kichaka, "Mose! Mose!"
Naye Mose akajibu, "Mimi hapa."
5 Mungu akamwambia, "Usikaribie zaidi. Vua viatu vyako, kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu." 6 Kisha akamwambia, "Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo." Mose aliposikia hayo, akafunika uso wake kwa sababu aliogopa kumtazama Mungu.