Publicidade

Isaías 15

Unabii Dhidi Ya Moabu

1 Neno kuhusu Moabu:

Ari iliyo Moabu imeangamizwa:

imeharibiwa kwa usiku mmoja!

Kiri iliyo Moabu imeangamizwa,

imeharibiwa kwa usiku mmoja!

2 Diboni anakwea hadi kwenye hekalu lake,

mpaka mahali pake pa juu ili walie,

Moabu anaombolezea Nebo na Medeba.

Kila kichwa kimenyolewa

na kila ndevu limeondolewa.

3 Wamevaa nguo za magunia barabarani,

juu ya mapaa na kwenye viwanja

wote wanaomboleza,

wamelala kifudifudi kwa kulia.

4 Heshboni na Eleale wanalia,

sauti zao zinasikika hadi Yahazi.

Kwa hiyo watu wenye silaha wa Moabu wanapiga kelele,

nayo mioyo yao imezimia.

5 Moyo wangu unamlilia Moabu;

wakimbizi wake wanakimbilia Soari,

hadi Eglath-Shelishiya.

Wanapanda njia ya kwenda Luhithi,

wanakwenda huku wanalia;

barabarani iendayo Horonaimu

wanaombolezea maangamizi yao.

6 Maji ya Nimrimu yamekauka

na majani yamenyauka;

mimea imekauka wala hakuna

kitu chochote kibichi kilichobaki.

7 Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba

wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi.

8 Mwangwi wa kilio chao umefika hadi mpakani mwa Moabu,

kilio chao cha huzuni kimefika hadi Eglaimu,

maombolezo yao hadi Beer-Elimu.

9 Maji ya Dimoni yamejaa damu,

lakini bado nitaleta pigo jingine juu ya Dimoni:

simba juu ya wakimbizi wa Moabu

na juu ya wale wanaobaki katika nchi.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-15_21-32-39-