3 Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona?
Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’
"Lakini katika siku ya kufunga kwenu, mnafanya mnavyotaka
na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote.
4 Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano,
na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu.
Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo
na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu.
5 Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua,
siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza?
Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete,
na kwa kujilaza juu ya nguo ya gunia na majivu?
Je, huo ndio mnaouita mfungo,
siku iliyokubalika kwa Bwana?
6 "Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua:
kufungua minyororo ya udhalimu,
na kufungua kamba za nira,
kuwaweka huru walioonewa,
na kuvunja kila nira?