Kitabu na Mwana-Kondoo
1 Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na nje, kikiwa kimefungwa kwa mihuri saba. 2 Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, "Ni nani anayestahili kuivunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu?" 3 Lakini hapakuwa na yeyote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala hata kutazama ndani yake. 4 Nikalia sana kwa sababu hakuonekana yeyote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake. 5 Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, "Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja mihuri yake saba."
6 Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba5:6 Roho saba za Mwenyezi Mungu hapa inamaanisha Roho wa Mungu katika ukamilifu wa utendaji wake. za Mungu zilizotumwa duniani pote.