Publicidade

Ezequiel 7

Mwisho umewadia

1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2 "Mwanadamu, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa nchi ya Israeli:

" ‘Mwisho! Mwisho umekuja

juu ya pembe nne za nchi!

3 Sasa mwisho umekuja juu yenu,

nami nitamwaga hasira yangu dhidi yenu.

Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu

na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za kuchukiza.

4 Sitawaonea huruma

wala kuwarehemu.

Hakika nitawalipiza kwa ajili ya matendo yenu

na desturi za machukizo miongoni mwenu.

Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’

5 "Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:

" ‘Maafa! Maafa ambayo hayajasikiwa!

Tazama, yanakuja!

6 Mwisho umewadia!

Mwisho umewadia!

Umejiinua wenyewe dhidi yenu.

Tazama, umewadia!

7 Maangamizi yamekuja juu yenu,

ninyi mnaoishi katika nchi.

Wakati umewadia! Siku imekaribia!

Kuna hofu kuu ya ghafula juu ya milima, wala si furaha.

8 Ninakaribia kumwaga ghadhabu yangu juu yenu

na kumaliza hasira yangu dhidi yenu.

Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu

na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za machukizo.

9 Sitawaonea huruma

wala kuwarehemu.

Nitawalipiza kwa ajili ya matendo yenu

na desturi za machukizo miongoni mwenu.

" ‘Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu ambaye huwapiga.

10 " ‘Tazama, siku imefika!

Tazama, imewadia!

Maangamizi yamezuka ghafula,

fimbo imechanua,

nayo majivuno yamechipua!

11 Jeuri imeinuka

kuwa fimbo ya kuadhibu waovu.

Hakuna hata mmoja wa hao watu atakayeachwa,

hata mmoja wa kundi hilo:

hakuna utajiri wao utabaki,

wala chochote cha thamani.

12 Wakati umewadia,

siku imefika.

Mnunuzi na asifurahi

wala muuzaji asihuzunike,

kwa maana ghadhabu iko juu ya kundi lote.

13 Muuzaji hatajipatia tena

ardhi aliyoiuza

wakati wote wawili wangali hai.

Kwa kuwa maono kuhusu kundi lote

hayatatanguka.

Kwa sababu ya dhambi zao, hakuna hata mmoja

atakayeokoa maisha yake.

14 " ‘Wajapopiga tarumbeta

na kuweka kila kitu tayari,

hakuna hata mmoja atakayeenda vitani,

kwa maana ghadhabu yangu iko juu ya kundi lote.

15 Nje ni upanga,

ndani ni tauni na njaa.

Walio shambani

watakufa kwa upanga,

nao waliomo mjini

njaa na tauni vitawala.

16 Wote watakaopona

na kutoroka watakuwa milimani,

wakiomboleza kama hua wa mabondeni,

kila mmoja kwa sababu ya dhambi zake.

17 Kila mkono utalegea

na kila goti litakuwa dhaifu kama maji.

18 Watavaa gunia

na kufunikwa na hofu.

Nyuso zao zitafunikwa na aibu,

na vichwa vyao vitanyolewa.

19 " ‘Watatupa fedha yao barabarani,

nayo dhahabu yao itakuwa najisi.

Fedha yao na dhahabu yao

havitaweza kuwaokoa

katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.

Hawatashibisha njaa yao

au kujaza tumbo zao kwa hiyo fedha wala dhahabu,

kwa sababu imewaponza wajikwae dhambini.

20 Walijivunia vito vyao vizuri

na kuvitumia kutengeneza sanamu za machukizo

na vinyago vya upotovu.

Kwa hiyo nitavifanya vitu hivyo kuwa najisi kwao.

21 Nitavitia vyote mikononi mwa wageni

kuwa nyara na kuwa vitu vilivyotekwa mikononi mwa watu waovu wa dunia,

nao watavinajisi.

22 Nitaugeuza uso wangu mbali nao,

nao waovu wa dunia watapanajisi mahali pangu pa thamani.

Wanyang’anyi watapaingia

na kupanajisi.

23 " ‘Andaa minyororo,

kwa sababu nchi imejaa umwagaji wa damu

na mji umejaa udhalimu.

24 Nitaleta taifa ovu kuliko yote

kumiliki nyumba zao.

Nitakomesha kiburi cha wenye nguvu

na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi.

25 Hofu ya ghafula itakapokuja,

watatafuta amani, lakini haitapatikana.

26 Maafa juu ya maafa yatakuja,

tetesi ya mabaya juu ya tetesi ya mabaya.

Watajitahidi kupata maono kutoka kwa nabii;

mafundisho ya sheria toka kwa kuhani yatapotea,

vivyo hivyo shauri kutoka kwa wazee.

27 Mfalme ataomboleza,

mwana wa mfalme atavikwa kukata tamaa,

nayo mikono ya watu wa nchi itatetemeka.

Nitawaadhibu kulingana na matendo yao,

na kwa kanuni zao wenyewe nitawahukumu.

" ‘Ndipo watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ "

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-18_12-43-22-