Isa awanawisha wanafunzi wake miguu
1 Sikukuu ya Pasaka ilikuwa imekaribia. Isa alijua kuwa wakati wake wa kuondoka ulimwenguni ili kurudi kwa Baba13:1 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. umewadia. Alikuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni; naam, aliwapenda hadi mwisho.
2 Isa alipokuwa akila chakula cha jioni na wanafunzi wake, ibilisi alikuwa amekwisha kutia wazo la kumsaliti Isa ndani ya moyo wa Yuda Iskariote, mwana wa Simoni. 3 Isa, akijua kwamba Baba ameweka vitu vyote chini ya mamlaka yake, na kwamba yeye alitoka kwa Mungu na alikuwa anarudi kwa Mungu, 4 aliondoka chakulani, akavua vazi lake la nje, akajifunga kitambaa kiunoni. 5 Kisha akamimina maji kwenye sinia na kuanza kuwanawisha wanafunzi wake miguu na kuikausha kwa kile kitambaa alichokuwa amejifunga kiunoni.
6 Alipomfikia Simoni Petro, Petro akamwambia, "Bwana, je, wewe utaninawisha mimi miguu?"
7 Isa akamjibu, "Hivi sasa hutambui lile ninalofanya, lakini baadaye utaelewa."
8 Petro akamwambia, "La, wewe hutaninawisha miguu kamwe."
Isa akamjibu, "Kama nisipokunawisha, wewe huna sehemu nami."
9 Ndipo Simoni Petro akajibu, "Usininawishe miguu peke yake, Bwana, bali pamoja na mikono na kichwa pia!"
10 Isa akamjibu, "Mtu aliyekwisha kuoga anahitaji kunawa miguu tu, kwani mwili wake wote ni safi. Ninyi ni safi, ingawa si kila mmoja wenu." 11 Kwa kuwa yeye alijua ni nani ambaye angemsaliti, ndiyo sababu akasema si kila mmoja aliyekuwa safi.
12 Alipomaliza kuwanawisha miguu yao, alivaa tena mavazi yake, akarudi alikokuwa ameketi. Akawauliza, "Je, mmeelewa nililowafanyia? 13 Ninyi mnaniita mimi ‘Mwalimu’ na ‘Bwana’; hii ni sawa, maana ndivyo nilivyo. 14 Kwa hiyo, ikiwa mimi niliye Bwana wenu na Mwalimu wenu nimewanawisha ninyi miguu, pia hamna budi kunawishana miguu ninyi kwa ninyi. 15 Mimi nimewawekea kielelezo kwamba imewapasa kutenda kama vile nilivyowatendea ninyi. 16 Amin, amin nawaambia, mtumishi si mkuu kuliko bwana wake, wala aliyetumwa si mkuu kuliko yule aliyemtuma. 17 Sasa kwa kuwa mmejua mambo haya, heri kwenu mkiyatenda.