Publicidade

Joel 2

Jeshi la nzige

1 Pigeni tarumbeta katika Sayuni;

pigeni mbiu katika mlima wangu mtakatifu.

Wote wanaoishi katika nchi na watetemeke,

kwa kuwa siku ya Mwenyezi Mungu inakuja. Iko karibu,

2 siku ya giza na huzuni,

siku ya mawingu na utusitusi.

Kama mapambazuko yanavyosambaa

toka upande huu wa milima

hata upande mwingine,

jeshi kubwa na lenye nguvu linakuja.

Jambo kama hili halijakuwepo tangu zamani,

wala halitakuwepo tena kamwe

kwa vizazi vijavyo.

3 Mbele yao moto unateketeza,

nyuma yao miali ya moto

inawaka kwa nguvu.

Mbele yao nchi iko kama bustani ya Edeni,

nyuma yao ni jangwa lisilofaa:

hakuna kitu kinachowaepuka.

4 Wanaonekana kama farasi;

wanaenda mbio

kama askari wapanda farasi.

5 Wanatoa sauti kama magari ya vita,

wanaporukaruka juu ya vilele vya milima,

kama mlio wa miali ya moto ilayo mabua,

kama jeshi kubwa lililojipanga kwa ajili ya vita.

6 Wanapoonekana, mataifa yanakuwa katika maumivu makuu;

kila uso unabadilika rangi.

7 Wanashambulia kama mashujaa;

wanapanda kuta kama askari.

Wote wanatembea katika safu,

hawapotoshi safu zao.

8 Hakuna anayemsukuma mwenzake;

kila mmoja anaenda mbele moja kwa moja.

Wanapita katika vizuizi

bila kuharibu safu zao.

9 Wanaenda kasi kuingia mjini;

wanakimbia ukutani.

Wanaingia ndani ya nyumba;

kwa kuingilia madirishani kama wezi.

10 Mbele yao dunia inatikisika,

anga linatetemeka,

jua na mwezi vinatiwa giza,

na nyota hazitoi mwanga wake tena.

11 Mwenyezi Mungu anatoa mshindo wa ngurumo

mbele ya jeshi lake;

majeshi yake hayana idadi,

ni wenye nguvu nyingi

wale ambao hutii agizo lake.

Siku ya Mwenyezi Mungu ni kuu,

ni ya kutisha.

Ni nani anayeweza kuistahimili?

Rarueni mioyo yenu

12 "Hata sasa," asema Mwenyezi Mungu,

"nirudieni kwa mioyo yenu yote,

kwa kufunga, kwa kulia na kuomboleza."

13 Rarueni mioyo yenu

na siyo mavazi yenu.

Mrudieni Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,

kwa maana yeye ndiye mwenye neema

na mwingi wa huruma,

si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo,

huona huruma, hujizuia kuleta maafa.

14 Ni nani ajuaye? Yeye aweza kugeuka na kuwa na huruma

na kuacha baraka nyuma yake:

sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji

kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.

15 Pigeni tarumbeta katika Sayuni,

tangazeni saumu takatifu,

liiteni kusanyiko takatifu.

16 Wakusanyeni watu,

wekeni wakfu kusanyiko;

waleteni pamoja wazee,

wakusanyeni watoto,

wale wanyonyao maziwa.

Bwana arusi na atoke chumbani mwake

na bibi arusi naye atoke katika chumba chake.

17 Makuhani, ambao wanahudumu mbele za Mwenyezi Mungu,

na walie katikati ya ukumbi

wa Hekalu na madhabahu.

Waseme, "Wahurumie watu wako, Ee Mwenyezi Mungu.

Usifanye urithi wako kitu cha kudharauliwa,

neno la dhihaka kati ya mataifa.

Kwa nini wasemezane miongoni mwao,

‘Yuko wapi Mungu wao?’ "

Jibu la Mwenyezi Mungu

18 Kisha Mwenyezi Mungu atakuwa na wivu kwa ajili ya nchi yake

na kuwa na huruma juu ya watu wake.

19 Mwenyezi Mungu atawajibu:

"Ninawapelekea nafaka,

mvinyo mpya na mafuta,

vya kuwatosha ninyi

hadi mridhike kabisa;

kamwe sitawafanya tena

kitu cha kudharauliwa na mataifa.

20 "Nitafukuza jeshi la kaskazini likae mbali nanyi,

nikilisukuma ndani ya jangwa,

askari wa safu za mbele wakienda

ndani ya bahari ya mashariki

na wale wa safu za nyuma

katika bahari ya magharibi.

Uvundo wake utapaa juu;

harufu yake itapanda juu."

Hakika ametenda mambo makubwa.

21 Usiogope, ee nchi;

furahi na kushangilia.

Hakika Mwenyezi Mungu ametenda mambo makubwa.

22 Msiogope, enyi wanyama pori,

kwa kuwa mbuga za malisho yenu

zinarudia ubichi.

Miti nayo inazaa matunda,

mtini na mzabibu inatoa utajiri wake.

23 Furahini, enyi watu wa Sayuni,

shangilieni katika Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,

kwa kuwa amewapa mvua za vuli

kwa kipimo cha haki.

Anawapelekea mvua nyingi,

mvua ya vuli na ya masika, kama mwanzoni.

24 Sakafu za kupuria zitajaa nafaka,

mapipa yatafurika mvinyo mpya na mafuta.

25 "Nitawalipa kwa ajili ya miaka ile iliyoliwa na nzige:

parare, madumadu na tunutu,

jeshi langu kubwa ambalo

nililituma kati yenu.

26 Mtakuwa na wingi wa vyakula hadi mshibe,

na mtalisifu jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,

ambaye amefanya maajabu kwa ajili yenu;

kamwe watu wangu hawataaibishwa tena.

27 Ndipo mtajua kuwa mimi niko katika Israeli,

kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu,

na kwamba hakuna mwingine;

kamwe watu wangu hawataaibika tena.

Siku ya Mwenyezi Mungu

28 "Hata itakuwa, baada ya hayo,

nitamimina Roho wangu Mtakatifu juu ya wote wenye mwili.

Wana wenu wa kiume na wa kike watatabiri,

wazee wenu wataota ndoto,

na vijana wenu wataona maono.

29 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,

katika siku zile nitamimina Roho wangu Mtakatifu.

30 Nami nitaonesha maajabu katika mbingu

na duniani:

damu, moto na mawimbi ya moshi.

31 Jua litageuzwa kuwa giza

na mwezi kuwa mwekundu kama damu,

kabla ya kuja siku ya Mwenyezi Mungu

ile kuu na ya kutisha.

32 Na kila mtu atakayeliitia

jina la Mwenyezi Mungu ataokolewa.

Kwa maana juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu

kutakuwa na wokovu,

kama Mwenyezi Mungu alivyosema,

miongoni mwa walionusurika

ambao Mwenyezi Mungu awaita.

Veja também

Publicidade
Joel
Ver todos os capítulos de Joel
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-15_21-32-39-