13 Ilipokaribia wakati wa Pasaka ya Wayahudi, Isa alipanda kwenda Yerusalemu. 14 Huko uani la Hekalu aliwakuta watu wakiuza ng’ombe, kondoo na njiwa, nao wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha. 15 Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka ua la Hekalu, pamoja na kondoo na ng’ombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao. 16 Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, "Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?"
17 Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: "Wivu wa nyumba yako utanila."