Katika nyumba ya mfinyanzi
1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu: 2 "Shuka uende hadi nyumba ya mfinyanzi, nami huko nitakupa ujumbe wangu." 3 Kwa hiyo nikashuka hadi nyumba ya mfinyanzi, nikamkuta akifinyanga kwa gurudumu lake. 4 Lakini chombo alichokuwa akikifinyanga kutokana na udongo kilivunjika mikononi mwake; hivyo mfinyanzi akakifanya kuwa chombo kingine, umbo jingine kwa namna alivyoona ni vyema machoni pake.
5 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 6 "Ee nyumba ya Israeli, je, siwezi kuwafanyia kama huyu mfinyanzi afanyavyo?" asema Mwenyezi Mungu. "Kama vile udongo ulivyo katika mikono ya mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, ee nyumba ya Israeli.