59 Siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto, wakataka yule mtoto aitwe Zakaria, ambalo ndilo jina la baba yake. 60 Lakini mama yake akakataa na kusema, "Hapana! Jina lake ataitwa Yahya."
61 Wakamwambia, "Hakuna mtu yeyote katika jamaa yako mwenye jina kama hilo."
62 Basi wakamfanyia Zakaria baba yake ishara ili kujua kwamba yeye angependa kumpa mtoto jina gani. 63 Akaomba wampe kibao cha kuandikia na kwa mshangao wa kila mtu akaandika: "Jina lake ni Yahya." 64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kuongea, huku akimsifu Mungu.