Isa amponya mtu aliyekuwa kiziwi na bubu
31 Kisha Isa akaondoka sehemu za Tiro, akapita katikati ya Sidoni, hadi Bahari ya Galilaya na kuingia eneo la Dekapoli. 32 Huko, watu wakamletea Isa mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu.
33 Isa akampeleka yule kiziwi kando, mbali na watu, akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. 34 Ndipo Isa akatazama mbinguni, akashusha pumzi kwa nguvu, akamwambia, "Efatha!" (yaani, "Funguka!") 35 Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiliwa, akaanza kuongea sawasawa.
36 Isa akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hizi. Lakini kadiri alivyowakanya, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii. 37 Walistaajabu mno. Wakasema, "Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!"