Publicidade

Naum 3

Ole wa Ninawi

1 Ole wa mji unaomwaga damu,

uliojaa uongo,

uliojaa nyara,

na usiokosa mateka.

2 Kelele za mijeledi,

vishindo vya magurudumu,

farasi wanaoenda mbio

na mshtuo wa magari ya vita!

3 Wapanda farasi wanaenda mbio,

panga zinametameta,

na mikuki inang’aa!

Majeruhi wengi,

malundo ya maiti,

idadi ya miili isiyohesabika,

watu wanajikwaa juu ya mizoga:

4 haya yote kwa sababu ya wingi wa tamaa za kahaba,

anayeshawishi, bibi mkuu wa mambo ya uchawi,

anayewatia utumwani mataifa kwa ukahaba wake

na pia jamaa za watu kwa ulozi wake.

5 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anasema,

"Mimi ni kinyume na ninyi.

Nitafunika uso wako kwa gauni lako.

Nitaonesha mataifa uchi wako

na falme aibu yako.

6 Nitakutupia uchafu,

nitakufanyia dharau

na kukufanya kioja.

7 Wote wanaokuona watakukimbia na kusema,

‘Ninawi inaangamia,

nani atakayeomboleza kwa ajili yake?’

Nitampata wapi yeyote wa kukufariji?"

8 Je, wewe ni bora kuliko No-Amoni,

uliopo katika Mto Naili,

uliozungukwa na maji?

Mto ulikuwa kinga yake,

nayo maji yalikuwa ukuta wake.

9 Kushi na Misri walikuwa nguvu zake zisizo na mpaka;

Putu na Libia walikuwa miongoni mwa wale walioungana naye.

10 Hata hivyo alichukuliwa mateka

na kwenda uhamishoni.

Watoto wake wachanga walivunjwa vunjwa vipande

kwenye mwanzo wa kila barabara.

Kura zilipigwa kwa watu wake wenye heshima,

na watu wake wote wakuu walifungwa kwa minyororo.

11 Wewe pia utalewa;

utaenda mafichoni

na kutafuta kimbilio kutoka kwa adui.

12 Ngome zako zote ni kama mitini

yenye matunda yake ya kwanza yaliyoiva;

wakati inapotikiswa,

tini huanguka kwenye kinywa chake alaye.

13 Tazama vikosi vyako:

wote ni wanawake!

Malango ya nchi yako

yamekuwa wazi kwa adui zako;

moto umeteketeza mapingo yake.

14 Teka maji kwa ajili ya kuzingirwa kwako,

imarisha ulinzi wako,

Ufanyie udongo wa mfinyanzi kazi,

yakanyage matope,

karabati tanuru la kuchomea matofali!

15 Huko moto utakuteketeza,

huko upanga utakuangusha chini

na kama vile panzi, watakumaliza.

Ongezeka kama panzi,

ongezeka kama nzige!

16 Umeongeza idadi ya wafanyabiashara wako

hata wamekuwa wengi kuliko nyota za angani,

lakini kama nzige wanaacha nchi tupu

kisha huruka na kwenda zake.

17 Walinzi wako ni kama nzige,

maafisa wako kama makundi ya nzige

wanaotua kwenye kuta wakati wa siku ya baridi;

lakini wakati jua linapotokea wanaruka kwenda zao,

na hakuna anayejua wanakoenda.

18 Ee mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wanasinzia;

wakuu wako wanalala chini mavumbini kupumzika.

Watu wako wametawanyika juu ya milima

bila kuwa na mtu yeyote wa kuwakusanya.

19 Hakuna kitu kinachoweza kuponya jeraha lako;

jeraha lako ni la kukuua.

Kila anayesikia habari zako,

hupiga makofi kwa kuanguka kwako,

kwa kuwa ni nani ambaye hajaguswa

na ukatili wako usio na mwisho?

Veja também

Publicidade
Naum
Ver todos os capítulos de Naum
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_18-40-07-