Publicidade

Oséias 5

Hukumu dhidi ya Israeli

1 "Sikieni hili, enyi makuhani!

Kuweni wasikivu, enyi Waisraeli!

Sikieni, ee nyumba ya mfalme!

Hukumu hii ni dhidi yenu:

Mmekuwa mtego huko Mispa,

wavu uliotandwa juu ya Tabori.

2 Waasi wamezidisha sana mauaji.

Mimi nitawatiisha wote.

3 Ninajua yote kuhusu Efraimu,

Israeli hukufichika kwangu.

Efraimu, sasa umegeukia ukahaba,

Israeli amenajisika.

4 "Matendo yao hayawaachii

kurudi kwa Mungu wao.

Roho ya ukahaba iko ndani ya mioyo yao,

hawamkubali Mwenyezi Mungu.

5 Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao;

Waisraeli, hata Efraimu,

wanajikwaa katika dhambi zao;

pia Yuda atajikwaa pamoja nao.

6 Wanapoenda na makundi yao ya kondoo na ng’ombe

kumtafuta Mwenyezi Mungu,

hawatampata;

yeye amejiondoa kutoka kwao.

7 Wao si waaminifu kwa Mwenyezi Mungu;

wamezaa watoto haramu.

Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi

zitawaangamiza wao

pamoja na mashamba yao.

8 "Pigeni tarumbeta huko Gibea,

na baragumu huko Rama.

Pazeni kelele za vita huko Beth-Aveni;

ongoza, ee Benyamini.

9 Efraimu ataachwa ukiwa

katika siku ya kuadhibiwa.

Miongoni mwa makabila ya Israeli

ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia.

10 Viongozi wa Yuda ni kama wale

wanaosogeza mawe ya mpaka.

Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao

kama mafuriko ya maji.

11 Efraimu amedhulumiwa,

amekanyagwa katika hukumu

kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu.

12 Mimi ni kama nondo kwa Efraimu,

na kama uozo kwa watu wa Yuda.

13 "Efraimu alipoona ugonjwa wake,

naye Yuda vidonda vyake,

ndipo Efraimu aligeukia Ashuru,

na kuomba msaada kwa mfalme mkuu.

Lakini hawezi kukuponya,

hawezi kukuponya vidonda vyako.

14 Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu,

kama simba mkubwa kwa Yuda.

Nitawararua vipande vipande na kuondoka;

nitawachukua mbali,

na hakuna wa kuwaokoa.

15 Kisha nitarudi mahali pangu

hadi watakapokubali kosa lao.

Nao watautafuta uso wangu;

katika taabu yao watanitafuta kwa bidii."

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_06-50-08-