Adhabu haiepukiki
1 Kut 32:11-14;Hes 14:13-19;1 Sam 7:5-9 Ndipo BWANA akaniambia, Hata wangesimama mbele zangu Musa na Samweli, moyo wangu usingewaelekea watu hawa; watupe, watoke mbele za macho yangu, wakaende zao. 2 Zek 11:9;Ufu 13:10 Kisha itakuwa, hapo watakapokuambia, Tutoke, tuende wapi? Utawaambia, BWANA asema hivi, Walioandikiwa kufa, watakwenda kufa; au kufa kwa upanga, watakufa kwa upanga; au kufa kwa njaa, watakufa kwa njaa, au kutekwa nyara, watakuwa mateka. 3 Law 26:16;Kum 28:26 Nami nitaamrisha juu yao namna nne, asema BWANA; upanga uue, na mbwa wararue, na ndege wa angani, na wanyama wakali wa nchi, wale na kuangamiza. 4 Eze 23:46;2 Fal 21:1-16;2 Nya 33:1-9 Nami nitawafanya kuwa kitu cha kutisha katika falme zote za duniani, kwa sababu ya Manase, mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda, kwa sababu ya mambo aliyoyatenda katika Yerusalemu. 5 Isa 51:19 Maana ni nani atakayekuhurumia, Ee Yerusalemu? Au ni nani atakayekulilia? Au ni nani atakayegeuka upande ili kuuliza habari za hali yako? 6 Hos 13:14 Umenikataa mimi, asema BWANA, umerudi nyuma; ndiyo maana nimenyosha mkono wangu juu yako, na kukuangamiza; nimechoka kwa kughairi. 7 Isa 9:13;Yer 5:3 Nami nimewapepea kwa kipepeo katika malango ya nchi nimewaondolea watoto wao, nimewaharibu watu wangu; hata hivyo hawakurudi na kuziacha njia zao. 8 Wajane wao wameongezeka kwangu kuliko mchanga wa bahari; nimeleta mwenye kuteka wakati wa adhuhuri juu ya mama wa vijana; nimeleta uchungu na hofu kuu impate ghafla. 9 1 Sam 2:5;Isa 47:9;Amo 8:9 Mwanamke aliyezaa watoto saba anazimia; ametoa roho; jua lake limekuchwa, ikiwa bado ni wakati wa mchana; ameaibika na kutwezwa; na mabaki yao nitawatoa kwa upanga mbele ya adui zao, asema BWANA.
Yeremia alalamika tena na kuhakikishiwa
10 Ayu 3:1 Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani. 11 BWANA akasema, Hakika nitakutia nguvu upate mema; hakika nitamlazimisha adui akusihi wakati wa uovu, na wakati wa taabu.
12 Je! Mtu aweza kuvunja chuma, naam, chuma kitokacho kaskazini, au shaba? 13 Zab 44:12;Isa 52:3;Yer 17:3 Mali yako na hazina zako nitazitoa kuwa nyara, bila kulipwa thamani yake; naam, kwa sababu ya dhambi zako zote, hata katika mipaka yako yote. 14 Kum 32:22 Nami nitakulazimisha kuwatumikia adui zako katika nchi usiyoijua; maana moto umewashwa katika hasira yangu, utakaowateketeza ninyi.
15 Ayu 10:7;Yn 21:15-17;Zab 17:3;69:7;Yer 12:3;11:20;Mt 5:10-12;1 Pet 4:14-16 Ee BWANA, unajua wewe; unikumbuke, unijie, ukanilipizie kisasi juu yao wanaoniudhi; usiniondoe kwa uvumilivu wako; ujue ya kuwa ni kwa ajili yako nilivyopatikana na matukano. 16 Eze 3:1;Ayu 23:12 Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee BWANA, Mungu wa majeshi. 17 Zab 1:1 Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi, niliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu. 18 Yer 30:15;Ayu 6:15 Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha langu halina dawa, linakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu?
19 Zek 3:7;Eze 22:26 Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejesha, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao. 20 Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema BWANA. 21 Isa 49:25 Nami nitakuokoa kutoka kwa mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa kutoka kwa mkono wao wenye kutisha.