1 Ikawa Yeremia alipokwisha kuwaambia watu wote maneno yote ya BWANA, Mungu wao, ambayo BWANA, Mungu wao, amemtuma kwao, yaani, maneno hayo yote, 2 ndipo Azaria, mwana wa Hoshaya, na Yohana mwana wa Karea, na watu wote wenye kiburi wakanena, wakimwambia Yeremia, Unasema uongo; BWANA, Mungu wetu, hakukutuma useme, Msiende Misri kukaa huko; 3 bali Baruku, mwana wa Neria, akushawishi kinyume chetu, ili kututia katika mikono ya Wakaldayo, ili watuue, na kutuchukua mateka mpaka Babeli. 4 Basi Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa majeshi, na watu wote hawakuitii sauti ya BWANA, kwamba wakae katika nchi ya Yuda. 5 Lakini Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa majeshi, wakawatwaa wote waliosalia wa Yuda, waliokuwa wamerudi kutoka mataifa yote walikofukuzwa, wakae katika Yuda; 6 wanaume, na wanawake, na watoto, na binti za mfalme, na kila mtu ambaye Nebuzaradani, mkuu wa askari walinzi, amemwacha pamoja na Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, pia na Yeremia, nabii, na Baruku, mwana wa Neria; 7 wakaingia nchi ya Misri; maana hawakuitii sauti ya BWANA; wakafika hadi Tapanesi. 8 Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia huko Tapanesi, kusema, 9 Twaa mawe makubwa mikononi mwako, ukayafiche ndani ya chokaa ya kazi ya matofali, penye maingilio ya nyumba ya Farao huko Tapanesi, machoni pa watu wa Yuda; 10 ukawaambie, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitatuma na kumtwaa Nebukadneza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu, nami nitaweka kiti chake cha enzi juu ya mawe haya niliyoyaficha; naye atatandaza hema yake ya fahari juu yake. 11 Naye atakuja, na kuipiga nchi ya Misri; watu walioandikiwa kufa watakufa, nao walioandikiwa kuwa mateka watakuwa mateka, nao walioandikiwa kupigwa kwa upanga watapigwa kwa upanga. 12 Nami nitawasha moto katika nyumba za miungu ya Misri, na kuziteketeza, na kuwachukua mateka; naye atajipamba kwa nchi ya Misri, kama vile mchungaji avaavyo nguo zake; naye atatoka huko na amani. 13 Naye atazivunja nguzo za Beth-shemeshi, iliyoko huko katika nchi ya Misri, na nyumba za miungu ya Misri ataziteketeza.
Publicidade
Jeremias 43
Kupelekwa Misri, Yeremia Aanya kuhusu hukumu
Veja também
Publicidade