21 Ndipo Musa akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, "Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka. 22 Chukueni kitawi cha hisopo, mkichovye kwenye damu iliyopo kwenye sinia, na kuipaka sehemu ya hiyo damu kwenye vizingiti, na kwenye miimo yote miwili ya milango. Mtu yeyote asitoke nje ya mlango wa nyumba yake hadi asubuhi. 23 Mwenyezi Mungu apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu juu ya vizingiti na kwenye miimo ya milango, naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zenu na kuwapiga ninyi.