Publicidade

Provérbios 27

1 Usijisifu kwa ajili ya kesho,

kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.

2 Mwache mwingine akusifu,

wala si kinywa chako mwenyewe;

mtu mwingine afanye hivyo

na si midomo yako mwenyewe.

3 Jiwe ni zito na mchanga ni mzigo,

lakini kukasirishwa na mpumbavu ni kuzito kuliko vyote viwili.

4 Hasira ni ukatili na ghadhabu kali ni gharika,

lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu?

5 Afadhali karipio la wazi

kuliko upendo uliofichika.

6 Majeraha kutoka kwa rafiki yaonesha uaminifu,

lakini adui huzidisha busu.

7 Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali,

bali kwa mwenye njaa

hata kile kilicho kichungu

kwake ni kitamu.

8 Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake,

ndivyo alivyo mtu atangatangaye

mbali na nyumbani mwake.

9 Manukato na uvumba huleta furaha moyoni,

nao uzuri wa rafiki huchipuka

katika ushauri wake wa uaminifu.

10 Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako,

tena usiende nyumbani mwa ndugu yako

wakati umepatwa na maafa.

Bora jirani wa karibu

kuliko ndugu aliye mbali.

11 Mwanangu, uwe na hekima,

nawe ulete furaha moyoni mwangu,

ndipo nitakapoweza kumjibu yeyote

anitendaye kwa dharau.

12 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,

bali mjinga huendelea mbele, naye hupata madhara.

13 Chukua vazi la yule awekaye dhamana

kwa ajili ya mgeni;

lishikilie liwe dhamana

kwa ajili ya mgeni.

14 Mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu

asubuhi na mapema,

itahesabiwa kuwa ni laana.

15 Mke mgomvi ni kama

matone yasiyokoma siku ya mvua.

16 Kumzuia ni kama kuuzuia upepo,

au kukamata mafuta kwa kiganja cha mkono.

17 Kama vile chuma kinoavyo chuma,

ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.

18 Yeye autunzaye mtini atakula tunda lake,

naye amtunzaye bwana wake ataheshimiwa.

19 Kama uso uonekanavyo kwenye maji,

ndivyo hivyo moyo wa mtu humwonesha alivyo.

20 Kuzimu na Uharibifu havishibi,

wala macho ya mwanadamu hayashibi.

21 Kalibu husafisha fedha na tanuru husafisha dhahabu,

bali mtu hupimwa kwa sifa anazopewa na watu.

22 Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu,

ukimtwanga kama nafaka kwa mchi,

hutauondoa upumbavu wake.

23 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako ya kondoo na mbuzi;

angalia ng’ombe wako kwa makini.

24 Kwa kuwa utajiri haudumu milele,

nalo taji halidumu vizazi vyote.

25 Wakati majani makavu yameondolewa

na mapya yamechipua,

nayo majani toka milimani yamekusanywa,

26 wana-kondoo watakupatia mavazi

na mbuzi thamani ya shamba.

27 Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi

kukulisha wewe na jamaa yako,

na kuwalisha wajakazi wako.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-18_06-35-37-