Publicidade

Provérbios 24

Msemo 20

1 Usiwaonee wivu watu waovu,

usitamani ushirika nao;

2 kwa maana mioyo yao hupanga mambo ya jeuri,

nayo midomo yao husema kuhusu kuleta madhara.

Msemo 21

3 Kwa hekima nyumba hujengwa,

nayo kupitia ufahamu huimarishwa;

4 kwa maarifa vyumba vyake hujazwa

vitu vya thamani na vya kupendeza.

Msemo 22

5 Mtu mwenye hekima ana uwezo mkubwa,

naye mtu mwenye maarifa huongeza nguvu,

6 kwa kufanya vita unahitaji uongozi

na kwa ushindi washauri wengi.

Msemo 23

7 Hekima i juu mno kwa mpumbavu,

katika kusanyiko langoni

hana lolote la kusema.

Msemo 24

8 Yeye apangaye mabaya

atajulikana kama mtu wa hila.

9 Mipango ya upumbavu ni dhambi,

watu huchukizwa na mwenye dhihaka.

Msemo 25

10 Ukikata tamaa wakati wa taabu,

jinsi gani nguvu zako ni kidogo!

11 Okoa wale wanaoongozwa kwenye kifo;

wazuie wote wanaojikokota

kuelekea machinjoni.

12 Mkisema, "Lakini hatukujua lolote kuhusu hili,"

je, yule apimaye mioyo halitambui hili?

Je, yule awalindaye maisha yenu halijui hili?

Je, hatamlipa kila mtu kulingana na aliyotenda?

Msemo 26

13 Ule asali mwanangu, kwa kuwa ni nzuri;

asali kutoka sega ni tamu kwa kuonja.

14 Ujue pia kwamba hekima ni tamu kwa nafsi yako:

Ukiipata, kuna matumaini kwako ya siku zijazo,

nalo tumaini lako halitakatiliwa mbali.

Msemo 27

15 Usivizie kama haramia afanyavyo ili kuyashambulia

makao ya mwenye haki,

wala usiyavamie makazi yake,

16 kwa maana ingawa mtu mwenye haki huanguka mara saba,

huinuka tena;

lakini waovu huangushwa chini na maafa.

Msemo 28

17 Usitazame kwa kufurahia adui yako aangukapo;

wakati anapojikwaa,

usiruhusu moyo wako ushangilie.

18 Mwenyezi Mungu asije akaona na kuchukia

akaiondoa ghadhabu yake mbali naye.

Msemo 29

19 Usikasirike kwa sababu ya wapotovu,

wala usiwaonee wivu waovu,

20 kwa maana mpotovu hana tumaini la siku zijazo,

nayo taa ya waovu itazimwa.

Msemo 30

21 Mwanangu, mche Mwenyezi Mungu na mfalme,

wala usijiunge na waasi,

22 kwa maana hao wawili watatuma maangamizi ya ghafula juu yao,

naye ni nani ajuaye maafa wawezayo kuleta?

23 Hii pia ni misemo ya wenye hekima:

Kuonesha upendeleo katika hukumu si vyema:

24 Yeyote amwambiaye mwenye hatia,

"Wewe huna hatia,"

makabila ya watu watamlaani,

na mataifa watamkana.

25 Bali itakuwa vyema kwa wale watakaowatia hatiani wenye hatia,

nazo baraka tele zitawajilia juu yao.

26 Jawabu la uaminifu

ni kama busu la mdomoni.

27 Maliza kazi zako za nje,

nawe uweke mashamba yako tayari,

baada ya hayo, jenga nyumba yako.

28 Usishuhudie dhidi ya jirani yako bila sababu,

au kutumia midomo yako kudanganya.

29 Usiseme, "Nitamtenda kama alivyonitenda mimi;

nitamlipiza mtu yule kwa kile alichonitendea."

30 Nilipita karibu na shamba la mvivu,

karibu na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili,

31 miiba ilikuwa imeota kila mahali,

ardhi ilikuwa imefunikwa na magugu, na

ukuta wa mawe ulikuwa umebomoka.

32 Nikatafakari moyoni mwangu lile nililoliona,

nami nikajifunza somo kutokana na niliyoyaona:

33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,

bado kukunja mikono kidogo upate kupumzika:

34 na umaskini utakuja juu yako kama mnyang’anyi,

na kupungukiwa kutakujia kama mtu mwenye silaha.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-18_14-04-22-