Publicidade

Jó 3

Ayubu anailaani siku aliyozaliwa

1 Baada ya jambo hili, Ayubu akafumbua kinywa chake na kuilaani siku ya kuzaliwa kwake.

2 Kisha akasema:

3 "Siku ya kuzaliwa kwangu na ipotelee mbali,

na usiku ule iliposemekana,

‘Mtoto wa kiume amezaliwa!’

4 Siku ile na iwe giza;

Mungu juu na asiiangalie;

nayo nuru isiiangazie.

5 Giza na kivuli kikuu viikalie tena;

wingu na likae juu yake;

weusi na uifunike nuru yake.

6 Usiku ule na ushikwe na giza nene;

usihesabiwe katika siku za mwaka,

wala usihesabiwe katika siku za mwezi wowote.

7 Usiku ule na uwe tasa;

sauti ya furaha na isisikike ndani yake.

8 Wale wanaozilaani siku na wailaani hiyo siku,

wale walio tayari kumwamsha Lewiathani.

9 Nyota zake za alfajiri na ziwe giza;

nao ungojee mwanga bila mafanikio,

wala usiione miali

ya mapambazuko,

10 kwa sababu huo usiku haukunifungia

mlango wa tumbo la mama yangu,

ili kuyaficha macho yangu

kutokana na taabu.

11 "Kwa nini sikuangamia wakati wa kuzaliwa?

Kwa nini sikufa nilipokuwa ninatoka tumboni?

12 Kwa nini pakawa na magoti ya kunipokea

na matiti ili nipate kunyonyeshwa?

13 Kwa maana sasa ningekuwa nimepumzika kwa amani.

Ningekuwa nimelala na kupumzika

14 pamoja na wafalme na washauri wa dunia,

waliojijengea mahali ambapo sasa ni magofu,

15 pamoja na watawala waliokuwa na dhahabu,

waliozijaza nyumba zao kwa fedha.

16 Au kwa nini sikufichwa ardhini kama mtoto aliyezaliwa mfu,

kama mtoto mchanga ambaye kamwe hakuuona mwanga?

17 Huko waovu huacha kusumbua

na huko waliochoka hupumzika.

18 Wafungwa nao hufurahia utulivu wao,

hawasikii tena sauti ya kukemea ya kiongozi wa watumwa.

19 Wadogo kwa wakubwa wamo humo,

na mtumwa ameachiwa huru kutoka kwa bwana wake.

20 "Mbona nuru inawaangazia wale walio taabuni,

na hao wenye uchungu kupewa uhai,

21 wale wanaotamani kifo ambacho hakiji,

wale wanaotafuta kufa zaidi ya kutafuta hazina iliyofichwa,

22 ambao hujawa na furaha,

na hushangilia wanapofika kaburini?

23 Kwa nini uhai hupewa mtu

ambaye njia yake imefichika,

ambaye Mungu amemzingira?

24 Kwa maana kulia kwangu kwa uchungu kwanijia badala ya chakula;

kusononeka kwangu kunamwagika kama maji.

25 Lile nililokuwa nikiogopa limenijia;

lile nililokuwa nikihofia limenipata.

26 Sina amani, wala utulivu;

sina pumziko, bali taabu tu."

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-18_14-04-22-