Hekima ni bora kupita vyote
1 Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba;
sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.
2 Ninawapa mafundisho ya maana,
kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.
3 Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu,
ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu,
4 baba alinifundisha akisema,
"Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote;
yashike maagizo yangu na wewe utaishi.
5 Pata hekima, pata ufahamu;
usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.
6 Usimwache hekima naye atakuweka salama;
mpende, naye atakulinda.