Kuzingirwa kwa Yerusalemu kwaoneshwa
1 Wewe nawe, mwanadamu, jipatie tofali uliweke mbele yako, kisha, chora juu yake mfano wa mji, yaani, Yerusalemu; 2 ukauhusuru, ukajenge ngome juu yake, na kufanya boma juu yake; ukaweke makambi juu yake, na kuweka magogo ya kuubomoa yauzunguke pande zote. 3 Isa 8:18;Eze 12:6,11;Mk 14:22;Lk 2:34;Yn 4:48 Kisha ukajipatie bamba la chuma, ukalisimamishe liwe ukuta wa chuma kati ya wewe na mji huo; ukaelekeze uso wako juu yake, nao utahusuriwa, nawe utauhusuru. Hili litakuwa ishara kwa nyumba ya Israeli.
4 Tena lala chini kwa ubavu wako wa kushoto, ukaweke huo uovu wa nyumba ya Israeli juu yake; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala juu yake, kwa kadiri hiyo utauchukua uovu wao. 5 Maana nimekuagizia miaka ya uovu wao iwe kwako hesabu ya siku, yaani, siku mia tatu na tisini; ndivyo utakavyouchukua uovu wa nyumba ya Israeli. 6 Tena utakapozitimiza hizo, utalala kwa ubavu wako wa kulia, nawe utauchukua uovu wa nyumba ya Yuda; siku arubaini, siku moja kwa mwaka mmoja, nimekuagizia. 7 Nawe utauelekeza uso wako, uelekee kuzingirwa kwa Yerusalemu, na mkono wako utakuwa haukuvikwa nguo, nawe utatoa unabii juu yake. 8 Eze 3:25 Na tazama, nitakutia pingu, wala hutageuka toka upande mmoja hata upande wa pili, hata utakapozitimiza siku za kuzingirwa kwako.
9 Pia ujipatie ngano, na shayiri, na kunde, na dengu, na mtama, na kusemethi, ukavitie vyote katika chombo kimoja, ukajifanyie mkate kwa vitu hivyo; kwa kadiri ya hesabu ya siku utakazolala ubavuni mwako; yaani, siku mia tatu na tisini utaula. 10 Na chakula chako utakachokula kitapimwa, shekeli ishirini kwa siku moja; utakila kwa wakati wake. 11 Nawe utakunywa maji kwa kuyapima, sehemu ya sita ya hini; utayanywa kwa wakati wake. 12 Nawe utakila kama mkate wa shayiri, nawe utakioka mbele ya macho yao juu ya mashonde yatokayo katika mwanadamu. 13 Dan 1:8;Hos 9:3 BWANA akasema, Hivyo ndivyo wana wa Israeli watakavyokula chakula chao, hali kimetiwa unajisi, kati ya mataifa nitakakowafukuza. 14 Eze 9:8;Mdo 10:14;Law 11:40;19:7;Kut 22:31;Kum 14:3;Isa 65:4 Ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, tazama, roho yangu haikutiwa unajisi; maana tangu ujana wangu hata sasa sijala nyamafu, wala iliyoraruliwa na wanyama; wala nyama ichukizayo haikuingia kinywani mwangu. 15 Ndipo akaniambia, Tazama, nimekupa mashonde ya ng’ombe badala ya mashonde ya mwanadamu, nawe utakipika chakula chako juu ya hayo. 16 Law 26:26;Zab 105:16;Isa 3:1;Kum 28:48;Eze 5:16;12:18,19;Zab 68:3;Omb 1:11 Tena akaniambia, Mwanadamu, tazama, nitalivunja tegemeo la chakula katika Yerusalemu; nao watakula mkate kwa kuupima, na kwa kuutunza sana; nao watakunywa maji kwa kuyapima, na kwa hofu; 17 Law 26:39;Eze 24:23 wapate kupungukiwa na mkate na maji, na kustaajabiana, na kukonda kwa sababu ya uovu wao.