1 Jinsi dhahabu ilivyoacha kung’aa,
Na dhahabu iliyo safi ilivyobadilika!
Mawe ya patakatifu yametupwa
Mwanzo wa kila njia.
2 2 Kor 4:7 Wana wa Sayuni wenye thamani,
Walinganao na dhahabu safi,
Jinsi wanavyodhaniwa kuwa vyombo vya udongo,
Kazi ya mikono ya mfinyanzi!
3 Ayu 39:14 Hata mbwamwitu hutoa matiti,
Huwanyonyesha watoto wao;
Binti ya watu wangu amekuwa mkali,
Mfano wa mbuni jangwani.
4 Zab 22:15 Ulimi wa mtoto anyonyaye
Wagandamana na kinywa chake kwa kiu;
Watoto wachanga waomba chakula,
Wala hakuna hata mmoja awamegeaye.
5 Ayu 24:8;Lk 15:16 Wale waliokula vitu vya anasa
Wameachwa peke yao njiani;
Wale waliokuzwa kuvaa nguo nyekundu
Wakumbatia jaa.
6 Mwa 19:24 Maana uovu wa binti ya watu wangu ni mkubwa
Kuliko dhambi ya Sodoma,
Uliopinduliwa kama katika dakika moja,
Wala mikono haikuwekwa juu yake.
7 Wakuu wake walikuwa safi kuliko theluji,
Walikuwa weupe kuliko maziwa;
Miili yao, walikuwa wekundu kuliko marijani,
Na umbo lao kama yakuti samawi.
8 Zab 102:5 Nyuso zao ni nyeusi kuliko makaa;
Hawajulikani katika njia kuu;
Ngozi yao yagandamana na mifupa yao
Imekauka, imekuwa kama mti.
9 Heri wale waliouawa kwa upanga
Kuliko wao waliouawa kwa njaa;
Maana hao husinyaa, wakichomwa
Kwa kukosa matunda ya mashamba.
10 Omb 2:20;Kum 28:57;Eze 5:10 Mikono ya wanawake wenye huruma
Imewatokosa watoto wao wenyewe;
Walikuwa ndio chakula chao
Katika uharibifu wa binti ya watu wangu.
11 Kum 32:22 BWANA ameitimiza ghadhabu yake,
Ameimimina hasira yake kali;
Naye amewasha moto katika Sayuni
Ulioiteketeza misingi yake.
12 Kum 29:24 Wafalme wa dunia hawakusadiki,
Wala wote wakaao duniani,
Ya kwamba mtesi na adui wangeingia
Katika malango ya Yerusalemu.
13 Yer 5:31;Mt 23:31 Ni kwa sababu ya dhambi za manabii wake
Na maovu ya makuhani wake,
Walioimwaga damu ya wenye haki
Katikati yake.
14 Yer 2:34 Hutangatanga njiani kama vipofu,
Wametiwa unajisi kwa damu;
Hata ikawa hakuna aliyeweza
Kuyagusa mavazi yao.
15 Watu waliwapigia kelele, Ondokeni, Uchafu,
Ondokeni, ondokeni, msiguse;
Walipokimbia na kutangatanga, watu walisema kati ya mataifa,
Hawatakaa hapa tena.
16 Omb 5:12 Hasira ya BWANA imewatenga,
Yeye hatawaangalia tena;
Hawakujali nafsi za wale makuhani,
Hawakuwaheshimu wazee wao.
17 2 Fal 24:7;Isa 20:5,6 Macho yetu yamechoka
Kwa kuutazamia bure msaada wetu;
Katika kungoja kwetu tumengojea taifa
Lisiloweza kutuokoa.
18 2 Fal 25:4;Yer 51:33 Wanatuvizia hatua zetu,
Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu;
Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia;
Maana mwisho wetu umefika.
19 Waliotufuatia ni wepesi
Kuliko tai za mbinguni;
Hao walitufuatia milimani,
Nao walituotea jangwani.
20 Mwa 2:7;Yer 52:9 Pumzi ya mianzi ya pua zetu, masihi4:20 Au, mtiwa mafuta (tazama 1 Sam 2:10). wa BWANA,
Alikamatwa katika marima yao;
Ambaye kwa habari zake tulisema,
Chini ya kivuli chake tutakaa kati ya mataifa.
21 Furahi, ushangilie, Ee binti Edomu,
Ukaaye katika nchi ya Usi;
Hata kwako kikombe kitapita,
Utalewa, na kujifanya uchi.
22 Adhabu ya uovu wako imetimia, Ee binti Sayuni;
Hatakuhamisha tena;
Atapatiliza uovu wako, Ee binti Edomu;
Atazivumbua dhambi zako.