Publicidade

Isaías 25

Sifa kwa Mwenyezi Mungu

1 Ee Mwenyezi Mungu, wewe ni Mungu wangu,

nitakutukuza na kulisifu jina lako,

kwa maana katika ukamilifu wa uaminifu

umetenda mambo ya ajabu,

mambo yaliyokusudiwa tangu zamani.

2 Umeufanya mji kuwa lundo la kifusi,

mji wenye ngome kuwa magofu,

ngome imara ya wageni kuwa si mji tena,

wala hautajengwa tena kamwe.

3 Kwa hiyo mataifa yenye nguvu yatakuheshimu,

miji ya mataifa katili itakuogopa wewe.

4 Umekuwa kimbilio la watu maskini,

kimbilio la mhitaji katika taabu yake,

hifadhi wakati wa dhoruba

na kivuli wakati wa hari.

Kwa maana pumzi ya wakatili

ni kama dhoruba ipigayo ukuta

5 na kama joto la jangwani.

Wewe wanyamazisha kelele ya wageni;

kama vile hari ipunguzwavyo na kivuli cha wingu,

ndivyo wimbo wa wakatili unyamazishwavyo.

6 Juu ya mlima huu Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ataandaa

karamu ya vinono kwa mataifa yote,

karamu ya mvinyo wa zamani,

nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana.

7 Juu ya mlima huu ataharibu

sitara ihifadhiyo mataifa yote,

kile kifuniko kifunikacho mataifa yote,

8 yeye atameza mauti milele.

Bwana Mungu Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote;

ataondoa aibu ya watu wake duniani kote.

Mwenyezi Mungu amesema hili.

9 Katika siku ile watasema,

"Hakika huyu ndiye Mungu wetu;

tulimtumaini, naye akatuokoa.

Huyu ndiye Mwenyezi Mungu, tuliyemtumaini;

sisi tushangilie na kufurahia katika wokovu wake."

10 Mkono wa Mwenyezi Mungu utatulia juu ya mlima huu,

bali Moabu atakanyagwa chini

kama majani makavu yakanyagwavyo kwenye shimo la mbolea.

11 Watakunjua mikono yao katikati yake,

kama vile mwogeleaji akunjuavyo mikono yake ili aogelee.

Mungu atashusha kiburi chao

licha ya ujanja wa mikono yao.

12 Atabomoa kuta ndefu za ngome yako

na kuziangusha chini,

atazishusha chini ardhini,

hadi mavumbini kabisa.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_06-50-08-