Publicidade

Isaías 52

1 Amka, amka, ee Sayuni,

jivike nguvu.

Vaa mavazi yako ya fahari,

ee Yerusalemu, mji mtakatifu.

Asiyetahiriwa na aliye najisi

hataingia kwako tena.

2 Jikung’ute mavumbi yako,

inuka, uketi kwenye kiti cha utawala, ee Yerusalemu.

Jifungue minyororo iliyo shingoni mwako,

ee Binti Sayuni uliye mateka.

3 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:

"Mliuzwa pasipo malipo,

nanyi mtakombolewa bila fedha."

4 Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:

"Hapo kwanza watu wangu walishuka Misri kuishi,

hatimaye, Ashuru wakawadhulumu.

5 "Basi sasa nina nini hapa?" asema Mwenyezi Mungu.

"Kwa kuwa watu wangu wamechukuliwa pasipo malipo,

nao wale wanaowatawala wanawadhihaki,"

asema Mwenyezi Mungu.

"Mchana kutwa

jina langu limetukanwa bila kikomo.

6 Kwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu;

kwa hiyo katika siku ile watajua

kwamba ndimi niliyetangulia kulisema.

Naam, ni mimi."

7 Tazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema

ilivyo mizuri juu ya milima,

wale wanaotangaza amani,

wanaoleta habari njema,

wanaotangaza wokovu,

wauambiao Sayuni,

"Mungu wako anatawala!"

8 Sikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao,

pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha.

Mwenyezi Mungu atakaporejea Sayuni,

wataliona kwa macho yao wenyewe.

9 Pazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja,

enyi magofu ya Yerusalemu,

kwa maana Mwenyezi Mungu amewafariji watu wake,

ameikomboa Yerusalemu.

10 Mkono mtakatifu wa Mwenyezi Mungu umefunuliwa

machoni pa mataifa yote,

nayo miisho yote ya dunia itaona

wokovu wa Mungu wetu.

11 Ondokeni, ondokeni, tokeni huko!

Msiguse kitu chochote kilicho najisi!

Tokeni kati yake mwe safi,

ninyi mchukuao vyombo vya Mwenyezi Mungu.

12 Lakini hamtaondoka kwa haraka,

wala hamtaenda kwa kukimbia;

kwa maana Mwenyezi Mungu atatangulia mbele yenu,

Mungu wa Israeli atakuwa mlinzi nyuma yenu.

Mateso na utukufu wa mtumishi

13 Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa hekima;

atatukuzwa, na kuinuliwa juu, na kukwezwa sana.

14 Kama walivyokuwa wengi

walioshangazwa naye,

kwani uso wake ulikuwa umeharibiwa sana

zaidi ya mtu yeyote

na umbo lake kuharibiwa

zaidi ya mfano wa mwanadamu:

15 hivyo atayashangaza mataifa mengi,

nao wafalme watafunga vinywa vyao kwa sababu yake.

Kwa kuwa yale ambayo hawakuambiwa, watayaona,

nayo yale wasiyoyasikia, watayafahamu.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_06-50-08-