Mwokozi pekee wa Israeli
1 Lakini sasa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu,
yeye aliyekuumba, ee Yakobo,
yeye aliyekuhuluku, ee Israeli:
"Usiogope kwa maana nimekukomboa,
nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu.
2 Unapopita kwenye maji makuu,
nitakuwa pamoja nawe,
unapopita katika mito ya maji,
hayatakugharikisha.
Utakapopita katika moto,
hutaungua,
miali ya moto haitakuunguza.
3 Kwa kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wako,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.
Ninaitoa Misri kuwa fidia yako,
Kushi na Seba badala yako.