1 "Haya! Njooni, ninyi nyote wenye kiu,
njooni kwenye maji;
nanyi ambao hamna fedha,
njooni, nunueni na mle!
Njooni, nunueni divai na maziwa
bila fedha na bila gharama.
2 Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula,
na kutaabikia kitu kisichoshibisha?
Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri,
nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono.
3 Tegeni sikio mje kwangu,
nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi.
Nitafanya agano la milele nanyi,
pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi.
4 Tazama, nimemfanya kuwa shahidi wa mataifa,
kiongozi na jemadari wa mataifa.
5 Hakika utaita mataifa usiyoyajua,
nayo mataifa yale yasiyokujua yataharakisha kukujia,
kwa sababu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako,
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli,
kwa maana amekutukuza."
6 Mtafuteni Mwenyezi Mungu maadamu anapatikana;
mwiteni maadamu yu karibu.