1 1 Sam 2:25;Mit 9:7,8 Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye;
Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.
2 Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake;
Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri.
3 Zab 39:1 Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake;
Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu.
4 Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu;
Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa.
5 Kol 3:9;Rum 12:9 Mwenye haki huchukia kusema uongo;
Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu.
6 Mit 11:3 Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake;
Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi.
7 Kuna mtu anayejitajirisha, lakini hana kitu;
Kuna anayejifanya kuwa maskini, lakini ana mali nyingi.
8 Fidia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake;
Bali mtu maskini hasikii ogofyo lolote.
9 Nuru ya mwenye haki yang’aa sana;
Bali taa ya mtu mbaya itazimika.
10 Kiburi huleta mashindano tu;
Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.
11 Mit 20:21 Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka;
Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.
12 Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua.
Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.
13 2 Nya 36:16 Kila anayelidharau neno hujiletea uharibifu;
Bali yeye anayeiogopa amri atapewa thawabu.
14 Mit 16:22;15:24;2 Sam 22:6;Zab 116:3 Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima,
Ili kuepukana na tanzi za mauti.
15 Ufahamu mwema huleta upendeleo;
Bali njia ya muasi huangamiza.
16 Mit 12:23 Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa;
Bali mpumbavu hueneza upumbavu.
17 Mjumbe mbaya huanguka maovuni;
Bali mjumbe mwaminifu ni afya.
18 Mit 15:5 Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa;
Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa.
19 Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu;
Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu.
20 Nenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima;
Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.
21 Zab 32:10 Uovu huwafuatia wenye dhambi;
Bali mwenye haki atalipwa mema.
22 Mhu 2:26 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi;
Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.
23 Mit 12:11 Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini;
Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma.
24 Mit 19:18;22:15 Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe;
Bali yeye ampendaye humrudi mapema.
25 Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake;
Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa.