1 Afadhali mego kavu pamoja na utulivu,
Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi.
2 Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu;
Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu.
3 Zab 26:2;Mit 27:21;Yer 17:10;Mal 3:3 Kalibu ni kwa fedha, na tanuri kwa dhahabu;
Bali BWANA huijaribu mioyo.
4 Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu;
Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara.
5 Ayu 31:29;Mit 24:17;Oba 1:12 Amchekaye maskini humtukana Muumba wake;
Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu.
6 Wana wa wana ndio taji la wazee,
Na utukufu wa watoto ni baba zao.
7 Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu;
Sembuse midomo ya uongo kinywani mwa mkuu.
8 Mwa 39:21;Dan 6:3 Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho;
Kila kigeukapo hufanikiwa.
9 Afunikaye kosa hutafuta kupendwa;
Bali yeye afichuaye siri hutenga rafiki.
10 Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu,
Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu.
11 Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu;
Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake.
12 Afadhali mtu akutwe na dubu jike aliyenyang’anywa watoto wake,
Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake.
13 Yer 18:20;Rum 12:17;1 The 5:15 Yeye arudishaye mabaya badala ya mema,
Mabaya hayataondoka nyumbani mwake.
14 Mit 20:3;Mdo 6:1;Rum 12:18;1 The 4:11 Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji;
Basi acheni ugomvi kabla haujafurika.
15 Kut 23:7;Isa 5:23 Yeye asemaye kwamba asiye haki ana haki;
naye asemaye kwamba mwenye haki hana haki;
Hao wote wawili ni chukizo kwa BWANA.
16 Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima,
Ikiwa hana moyo wa ufahamu?
17 Rafiki hupenda sikuzote;
Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.
18 Asiye na hekima hupeana mkono na mtu;
Na kuwa mdhamini wa mtu mwingine.
19 Apendaye ugomvi hupenda dhambi;
Auinuaye sana mlango wake hutafuta uharibifu.
20 Mtu mwenye moyo wa ukaidi hatapata mema;
Na mwenye ulimi wa upotovu huanguka katika misiba.
21 Azaaye mpumbavu ni kwa huzuni yake mwenyewe;
Wala baba wa mpumbavu hana furaha.
22 Moyo uliochangamka ni dawa nzuri;
Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa.
23 Kut 23:8 Asiye haki hutoa rushwa kifuani,
Ili kuzipotosha njia za hukumu.
24 Mhu 2:14 Hekima huwa machoni pake mwenye ufahamu;
Bali macho ya mpumbavu huwa katika ncha za dunia.
25 Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye,
Na uchungu kwa mamaye aliyemzaa.
26 Tena kumwadhibu mwenye haki si vizuri;
Wala si vyema kuwapiga wakuu kwa unyofu wao.
27 Yak 1:19 Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa;
Na mwenye roho ya utulivu ana busara.
28 Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima;
Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.