Koreshi ni chombo cha Mwenyezi Mungu
1 "Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kwa mpakwa mafuta wake,
Koreshi, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume
kutiisha mataifa mbele yake
na kuwavua wafalme silaha zao,
kufungua milango mbele yake
ili malango yasije yakafungwa:
2 Nitaenda mbele yako
na kusawazisha milima;
nitavunjavunja malango ya shaba
na kukatakata mapingo ya chuma.
3 Nitakupa hazina za gizani,
mali iliyofichwa mahali pa siri,
ili upate kujua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu,
Mungu wa Israeli, akuitaye kwa jina lako.