1 Ole wa nchi ya uvumi wa mabawa,
Iliyoko mbali kupita mito ya Kushi;
2 Ipelekayo wajumbe wake kwa njia ya bahari,
Na katika vyombo vya manyasi juu ya maji.
Nendeni, wajumbe wepesi, kwa watu warefu, laini;
Watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa;
Taifa la wenye nguvu, wakanyagao watu,
Ambao mito inakata nchi yao.
3 Enyi watu mkaao katika ulimwengu wote, na wenyeji wa dunia, bendera ikiinuliwa milimani, angalieni; na wakipiga tarumbeta, sikieni. 4 Maana BWANA ameniambia hivi, Mimi nitatulia, na kuangalia katika makazi yangu, kama wakati wa mwangaza mweupe wa jua kali, mfano wa wingu la umande katika joto la mavuno. 5 Maana kabla ya mavuno, maua yaangukapo, na maua yakawa zabibu zianzazo kuiva, ndipo atakapoyakata matawi kwa miundu, na kuviondoa vitawi vilivyopanuka na kuvikata. 6 Wote pamoja wataachiwa ndege wakali wa milimani, na wanyama wa nchi; ndege wakali watakaa juu yao wakati wa jua, na wanyama wote wa nchi watakaa juu yao wakati wa baridi. 7 Wakati huo BWANA wa majeshi ataletewa hidaya na watu warefu, laini;
Watu watishao tangu mwanzo wao hata sasa;
Taifa la wenye nguvu, wakanyagao watu,
Ambao mito inagawanya nchi yao;
Mpaka mahali pa jina la BWANA wa majeshi, mlima Sayuni.