Publicidade

Isaías 53

1 Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta?

Na mkono wa BWANA amefunuliwa nani?

2 Maana alikuwa mbele zake kama mche mwororo,

Na kama mzizi katika nchi kavu;

Yeye hana umbo wala uzuri;

Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.

3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu;

Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko;

Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,

Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.

4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu,

Amejitwika huzuni zetu;

Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa,

Amepigwa na Mungu, na kuteswa.

5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,

Alichubuliwa kwa maovu yetu;

Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake,

Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

6 Sisi sote kama kondoo tumepotea;

Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe;

Na BWANA ameweka juu yake

Maovu yetu sisi sote.

7 Alionewa, lakini alinyenyekea,

Wala hakufunua kinywa chake;

Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni,

Na kama vile kondoo anyamazavyo

Mbele yao wakatao manyoya yake;

Naam, hakufunua kinywa chake.

8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa;

Na maisha yake ni nani angeyajali?

Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai;

Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.

9 Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya;

Na pamoja na matajiri katika kufa kwake;

Ingawa hakutenda jeuri,

Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.

10 Lakini BWANA aliridhika kumchubua;

Amemhuzunisha;

Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi,

Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi,

Na mapenzi ya BWANA yatafanikiwa mkononi mwake;

11 Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika.

Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki

Atawafanya wengi kuwa wenye haki;

Naye atayachukua maovu yao.

12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu,

Naye atagawana nyara pamoja nao walio hodari;

Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa,

Akahesabiwa pamoja na hao wakosao.

Walakini alichukua dhambi za watu wengi,

Na kuwaombea wakosaji.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_18-40-07-