Pular para o conteúdo
Publicidade

Isaya 47

Kuaibishwa kwa Babeli

1 Yer 48:18;Omb 2:3,10; Isa 13:1—14:23; Yer 50:1—51:64 Haya, shuka, keti mavumbini,

Ewe bikira, binti Babeli;

Keti chini pasipo kiti cha enzi,

Ewe binti wa Wakaldayo;

Maana hutaitwa tena mwororo, mpenda anasa.

2 Kut 11:5 Twaa mawe ya kusagia, usage unga;

Vua utaji wako, ondoa mavazi yako,

Funua mguu wako, pita katika mito ya maji.

3 Nah 3:5;Mt 7:2;Rum 12:19 Uchi wako utafunuliwa,

Naam, aibu yako itaonekana.

Nitalipa kisasi; simkubali mtu yeyote.

4 Mkombozi wetu, BWANA wa majeshi ndilo jina lake,

Mtakatifu wa Israeli.

5 1 Sam 2:9;Dan 2:37 Kaa kimya, ingia gizani,

Ee binti wa Wakaldayo;

Maana hutaitwa tena Malkia wa falme.

6 2 Nya 28:9;Isa 10:6;Zek 1:15;Kum 28:50 Nilikuwa nimekasirika na watu wangu, niliutia unajisi urithi wangu, nikawatia mkononi mwako; wewe hukuwatendea rehema; kwa wazee uliifanya nira yako kuwa nzito sana. 7 Ufu 18:7 Ukasema, Mimi nitakuwa malkia milele; hata hukuyatia hayo moyoni mwako, wala hukukumbuka mwisho wa mambo hayo.

8 Sef 2:15;Ufu 18:7-8 Sasa, basi, sikia haya, wewe upendaye anasa, ukaaye na kujiona salama, wewe usemaye moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi; sitaketi kama mjane, wala sitajua kufiwa na watoto; 9 1 The 5:3;Dan 2:2;Nah 3:4;2 The 2:9,10;Ufu 9:21 lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kamili, uchawi wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno. 10 Zab 52:7;Eze 8:12 Maana umeutumainia ubaya wako; umesema, Hapana anionaye; hekima yako, na maarifa yako yamekupotosha, nawe umesema moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi. 11 Isa 13:6;Dan 5:30;Lk 17:27 Kwa sababu hiyo uovu utakupata; wala hutaweza kuuagua; na msiba utakuangukia; hutaweza kuuondoa; na ukiwa usioujua utakupata kwa ghafla. 12 Simama sasa na uganga wako, na wingi wa uchawi wako, uliojitaabisha nao tangu ujana wako; labda utaweza kupata faida, labda utaweza kushinda. 13 Umechoka kwa wingi wa mashauri yako; basi, na wasimame hao wanajimu, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe kutoka kwa mambo yatakayokupata. 14 Nah 1:10;Mal 4:1 Tazama, watakuwa kama mabua makavu; moto utawateketeza; hawatajiokoa kutoka kwa nguvu za muali wa moto; hili halitakuwa kaa la kujipasha moto, wala moto wa kuota. 15 Ufu 18:11 Ndivyo yatakavyokuwa mambo hayo uliyojitaabisha nayo; wale waliofanya biashara nawe tangu ujana wako watatangatanga mbali nawe, kila mtu akienda zake; hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.

Estes versículos te tocaram? Ore agora!

+581 estão orando agora.

Junte-se à corrente de oração.

Veja também