Ayubu ajibu: Malalamiko yangu ni machungu
1 Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2 Hata leo malalamiko yangu yana uchungu;
Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu.
3 Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona,
Nifike hata hapo anapokaa!
4 Ningeiweka kesi yangu mbele yake,
Na kukijaza kinywa changu hoja.
5 Ningeyajua maneno atakayonijibu,
Na kuelewa hayo atakayoniambia.
6 Ayu 9:19;Isa 27:4 Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake?
La, lakini angenisikiliza.
7 Hapo waelekevu wangepata kuhojiana naye;
Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele.
8 Zab 10:1;1 Tim 6:16 Tazama, naenda mbele, wala hayuko;
Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona;
9 Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona;
Hujificha upande wa kulia, hata nisimwone.
10 Zab 17:3;Yak 1:12 Lakini yeye aijua njia niendeayo;
Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.
11 Zab 44:18 Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake;
Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka.
12 Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake;
Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,
13 Ayu 34:29;Mhu 3:14;Rum 9:19;Yak 1:17 Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza?
Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo.
14 1 The 3:3 Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamriwa;
Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye.
15 Zab 119:120 Kwa hiyo naona taabu mbele ya uso wake;
Nitakapofikiri, namwogopa.
16 Kwa maana Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia,
Naye Mwenyezi amenitaabisha;
17 Ayu 6:9 Maana sikufadhaishwa kwa sababu ya giza,
Wala kwa sababu giza kuu limenifunika uso.