1 Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2 Hapana shaka ninyi ndinyi watu halisi,
Nanyi mtakapokufa, ndipo na hekima itakoma.
3 Lakini mimi pia, nina fahamu kama ninyi;
Mimi si duni kuliko ninyi;
Naam, ni nani asiyejua mambo kama hayo?
4 Mimi ni mtu wa kuchekwa na jirani yake,
Ni mtu niliyemwita Mungu, naye akanijibu;
Huyo mwenye haki, aliye mtimilifu, amekuwa ni kicheko.
5 Katika mawazo yake huyo aliye na raha mna kudharau balaa;
Tayari kwa ajili ya wenye kuteleza miguu.
6 Hema za wanyang'anyi hufanikiwa,
Na hao wamkasirishao Mungu hukaa salama;
Mikononi mwao Mungu huleta vitu vingi.
7 Lakini sasa waulize hao wanyama, nao watakufundisha;
Na ndege wa angani, nao watakuambia;
8 Au nena na nchi, nayo itakufundisha;
Nao samaki wa baharini watakutangazia.
9 Katika hawa wote ni yupi asiyejua,
Kwamba ni mkono wa BWANA uliofanya haya?
10 Ambaye nafsi ya kila kilicho hai i mkononi mwake,
Na pumzi zao wanadamu wote.
11 Je! Sikio silo lijaribulo maneno,
Kama vile kaakaa lionjavyo chakula?
12 Wazee ndio walio na hekima,
Na katika kuishi siku nyingi iko fahamu.
13 Hekima na amri zina yeye [Mungu];
Yeye anayo ushauri na fahamu.
14 Tazama, yuavunja, wala haiwezekani kujenga tena;
Humfunga mtu, wala haiwezekani kumfungua.
15 Tazama, yuayazuia maji, nayo yakatika;
Tena, huyatuma, nayo yaipindua dunia.
16 Kwake yeye ziko nguvu, na hekima;
Huyo adanganywaye, na mdanganyi pia ni wake.
17 Yeye huwaondoa washauri wakiwa wamevuliwa nguo,
Naye huwafanya waamuzi kuwa ni wapumbavu.
18 Yeye hulegeza kifungo cha wafalme,
Na kuwafunga viuno vyao kwa mshipi.
19 Yeye huwaondoa makuhani wakiwa wamevuliwa nguo.
Na kuwapindua mashujaa.
20 Huondoa usemi wa hao walioaminiwa,
Na kuondoa fahamu za wazee.
21 Humwaga aibu juu ya hao wakuu,
Na kulegeza mshipi wa wenye nguvu.
22 Huvumbua mambo ya siri tokea gizani,
Na hicho kilicho giza tupu huleta mwangani.
23 Huyaongeza mataifa, na kuyaangamiza;
Huyaeneza mataifa mbali, na kuyaacha.
24 Huwaondolea moyo wakuu wa watu wa nchi,
Na kuwapoteza nyikani pasipokuwa na njia.
25 Wao hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga,
Naye huwafanya kupepesuka kama mlevi.