1 Tena Elihu akajibu na kusema,
2 Sikilizeni maneno yangu, enyi wenye hekima;
Tegeni masikio kwangu, ninyi mlio na maarifa.
3 Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno,
Kama vile kaakaa lionjavyo chakula.
4 Na tujichagulie yaliyo ya uelekevu;
Na tujue wenyewe yaliyo mema.
5 Kwani Ayubu amesema, Mimi ni mwenye haki,
Naye Mungu ameniondolea haki yangu;
6 Nijapokuwa mwenye haki, nimehesabiwa kuwa mwongo;
Jeraha langu haliponyeki, nijapokuwa sina makosa.
7 Je! Ni mtu gani mfano wa Ayubu,
Anywaye mzaha kama maji?
8 Atembeaye na hao watendao uovu,
Na kwenda pamoja na watu wabaya.
9 Kwa kuwa amenena, Haimfai mtu lolote
Kujifurahisha na Mungu.
10 Kwa hiyo nisikilizeni, enyi wenye fahamu;
Mungu asidhaniwe kutenda udhalimu;
Wala Mwenyezi kufanya uovu.
11 Kwani atamlipa binadamu kwa kazi yake,
Naye atamfanya kila mtu kuona kulingana na njia zake.
12 Naam, hakika, Mungu hatatenda mabaya,
Wala Mwenyezi hatapotosha hukumu.
13 Ni nani aliyemwagiza kuiangalia dunia?
Au ni nani aliyemwekea ulimwengu huu wote?
14 Kama akimwekea mtu moyo wake,
Akijikusanyia roho yake na pumzi zake;
15 Wenye mwili wote wangeangamia pamoja,
Nao wanadamu watarejea tena kuwa mavumbi.
16 Ikiwa una ufahamu, sikia neno hili;
Isikilize sauti ya maneno yangu.
17 Je! Atatawala mtu aichukiaye haki hata mmoja?
Nawe, je! Utamhukumia mkosa aliye na haki na mwenye nguvu?
18 Je! Inafaa kumwambia mfalme, Wewe u mwovu?
Au kuwaambia wakuu, Ninyi ni wabaya?
19 Sembuse yeye huwajali nyuso za wakuu,
Wala hawajali matajiri kuliko maskini?
Kwani wote ni kazi ya mikono yake,
20 Hufa ghafla, hata usiku wa manane;
Watu hutikisika na kwenda zao,
Nao mashujaa huondolewa pasipo mkono wa mtu.
21 Kwani macho yake yako juu ya njia za mtu,
Naye huziona hatua zake zote.
22 Hapana hofu ya giza kuu,
mahali wawezapo kujificha watendao udhalimu.
23 Kwani yeye hana haja ya kumfikiria mtu zaidi,
ili aende mbele za Mungu ahukumiwe.
24 Yeye huwavunjavunja mashujaa pasipo kuwachunguza,
Na kuwaweka wengine mahali pao.
25 Kwa sababu hiyo yeye huyatafiti matendo yao;
Naye huwapindua usiku, wakaangamia.
26 Yeye huwapiga kwa sababu ya uovu wao,
Waziwazi mbele ya macho ya wengine;
27 Kwa sababu walikengeuka, wasimfuate yeye,
Wasikubali kuzishika njia zake hata moja;
28 Hata wakafanya kilio cha maskini kumfikia,
Naye akasikia kilio cha hao wateswao.
29 Akitoa utulivu yeye, ni nani awezaye kuhukumia makosa?
Akificha uso wake, ni nani awezaye kumtazama?
Kama hufanyiwa taifa, au mtu mmoja, ni sawasawa;
30 Ili huyo mpotovu asitawale,
Wala pasiwe na wa kuwatega watu.
31 Kwani kuna mtu aliyemwambia Mungu,
Mimi nimevumilia kurudiwa, ingawa sikukosa;
32 Nisiyoyaona nifundishe wewe;
Kama nimefanya uovu sitafanya tena?
33 Je! Malipo yake yatakuwa kama upendavyo wewe, hata ukayakataa?
Kwani yakupasa wewe kuchagua, si mimi;
Kwa sababu hiyo sema uyajuayo.
34 Watu walio na akili wataniambia,
Naam, kila mtu mwenye hekima anisikiaye;
35 Huyo Ayubu amesema pasipo maarifa,
Na maneno yake hayana hekima.
36 Laiti Ayubu angejaribiwa hadi mwisho,
Kwa kuwa amejibu kama watu waovu.
37 Maana huongeza uasi juu ya dhambi zake,
Apiga makofi kati yetu,
Na kuongeza maneno yake kinyume cha Mungu.