1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu, na kusema,
2 Je! Huu wingi wa maneno usijibiwe?
Na mtu aliyejaa maneno, je! Ahesabiwe kuwa na haki?
3 Je! Majivuno yako yawanyamazishe watu wawe kimya?
Nawe hapo ufanyapo dhihaka, je! Hapana mtu atakayekutahayarisha?
4 Kwa kuwa wewe wasema, Mafunzo yangu ni safi,
Nami ni safi machoni pako.
5 Lakini, laiti Mungu angenena,
Na kuifunua midomo yake juu yako;
6 Tena akuoneshe hizo siri za hekima,
Ya kuwa hufanikiwa katika kuyatimiza makusudi yake!
Ujue basi ya kuwa Mungu akuachilia katika uovu wako.
7 Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu?
Waweza kuufikia upeo wa huyo Mwenyezi?
8 Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe?
Ni wenye kina kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe?
9 Cheo chake ni kirefu kuliko dunia,
Ni kipana zaidi ya bahari.
10 Yeye akipita, na kufunga watu,
Na kuwaita hukumuni, ni nani basi awezaye kumzuia?
11 Kwa kuwa yeye awajua watu baradhuli;
Anapouona uovu, je; hatauangalia?
12 Lakini mpumbavu aweza kupata ufahamu,
Ingawa mwanadamu huzaliwa kama mtoto wa punda mwitu.
13 Wewe ukiuweka moyo wako kwa uelekevu,
Na kumnyoshea mikono yako;
14 Ikiwa una uovu mkononi mwako, uweke mbali nawe,
Wala usikubali upuzi kukaa hemani mwako;
15 Hakika ndipo utakapopata kuinua uso pasipo ila;
Naam, utathibitika, wala hutakuwa na hofu;
16 Kwa kuwa utasahau mateso yako;
Utayakumbuka kama maji yaliyokwisha pita;
17 Na maisha yako yatakuwa meupe kuliko adhuhuri;
Giza lake litakuwa kama alfajiri.
18 Nawe utakuwa salama, kwa sababu kuna matumaini;
Naam, utatafutatafuta kando yako, na kupumzika salama.
19 Tena utalala, wala hapana atakayekutia hofu;
Naam, wengi watakutafuta uso wako.
20 Lakini macho ya waovu yataingia kiwi,
Nao hawatakuwa na njia ya kukimbilia,
Na matumaini yao yatakuwa ni kutoa roho.