Publicidade

Jó 23

Ayubu ajibu: Malalamiko yangu ni machungu

1 Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2 Hata leo malalamiko yangu yana uchungu;

Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu.

3 Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona,

Nifike hata hapo anapokaa!

4 Ningeiweka kesi yangu mbele yake,

Na kukijaza kinywa changu hoja.

5 Ningeyajua maneno atakayonijibu,

Na kuelewa hayo atakayoniambia.

6 Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake?

La, lakini angenisikiliza.

7 Hapo waelekevu wangepata kuhojiana naye;

Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele.

8 Tazama, naenda mbele, wala hayuko;

Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona;

9 Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona;

Hujificha upande wa kulia, hata nisimwone.

10 Lakini yeye aijua njia niendeayo;

Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.

11 Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake;

Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka.

12 Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake;

Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,

13 Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza?

Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo.

14 Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamriwa;

Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye.

15 Kwa hiyo naona taabu mbele ya uso wake;

Nitakapofikiri, namwogopa.

16 Kwa maana Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia,

Naye Mwenyezi amenitaabisha;

17 Maana sikufadhaishwa kwa sababu ya giza,

Wala kwa sababu giza kuu limenifunika uso.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-18_14-04-22-