Publicidade

Jó 37

1 Moyo wangu hutetemeka kwa hayo pia,

Nao huruka kutoka mahali pake.

2 Zisikizeni hizo kelele za sauti yake,

Na uvumi utokao kinywani mwake.

3 Yeye huituma iende chini ya mbingu zote,

Na radi yake hata miisho ya nchi.

4 Baadaye sauti hunguruma;

Yeye hunguruma kwa sauti ya ukuu wake;

Hazizuii hapo sauti yake isikiwapo.

5 Mungu hunguruma kwa kustaajabisha kwa sauti yake;

Hufanya mambo makuu, ambayo hatuwezi kuyaelewa.

6 Kwa kuwa huiambia theluji, Anguka juu ya nchi;

Na pia kwa manyunyu ya mvua,

Hayo manyunyu ya mvua yake nyingi.

7 Huufunga mkono wa kila binadamu;

Ili watu wote aliowaumba wajue.

8 Hapo wanyama huingia mafichoni,

Na kukaa katika mapango yao.

9 Dhoruba hutoka katika vyumba vyake;

Na baridi ghalani mwake.

10 Kwa pumzi ya Mungu barafu hutokea;

Na uso wa maji huganda punde.

11 Naam, huyatwika mawingu mazito mzigo wa maji;

Hulitandika wingu la umeme wake;

12 Nalo hugeuzwa huku na huku kwa uongozi wake,

Ili yafanye yote atakayoyaagiza

Juu ya uso wa dunia hii ikaayo watu;

13 Kama ni kwa kuonya, au kama ni kwa nchi yake,

Au kama ni kwa rehema, ndiye aletaye.

14 Sikiliza neno hili, Ee Ayubu;

Simama kimya, uzifikiri kazi za Mungu za ajabu.

15 Je! Wajua wewe jinsi Mungu anavyoziagiza,

Na kuufanya umeme wa wingu lake uangaze?

16 Je! Wajua jinsi mawingu yalivyowekwa sawasawa,

Hizo kazi za ajabu za huyo mkamilifu wa maarifa?

17 Jinsi nguo zako zilivyo na moto,

Hapo nchi ituliapo kwa sababu ya upepo wa kusini?

18 Je! Waweza kuzitandaza mbingu pamoja naye,

Ambazo zina nguvu kama kioo cha kuyeyushwa?

19 Utufundishe ni maneno gani tutakayomwambia;

Kwa kuwa hatuwezi kutoa hoja zetu maana tumo gizani.

20 Je! Aambiwe kwamba nataka kunena?

Au kuna mtu ambaye angetamani kumezwa?

21 Na sasa watu hawawezi kuutazama mwanga ung'aao mbinguni;

Lakini upepo ukipita huzitakasa.

22 Kaskazini hutokea mng'ao wa dhahabu;

Mungu huvikwa ukuu utishao.

23 Yeye Mwenyezi hamwezi kumwona;

Yeye ni mkuu mwenye uweza;

Tena mwenye hukumu, na mwingi wa haki, hataonea.

24 Kwa hiyo watu humwogopa;

Yeye hawaangalii walio na hekima mioyoni.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-19_11-20-24-