1 Ayu 15:14;Zab 51:5;Mhu 2:23 Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke
Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu.
2 Isa 40:6;Yak 1:10;1 Pet 1:24 Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa;
Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.
3 Zab 144:3;143:2 Nawe, je! Wafumbua macho yako kumwangalia mtu kama yeye,
Na kunitia katika hukumu pamoja nawe?
4 Mwa 5:3;Zab 51:5;Yn 3:5;Rum 5:12;Efe 2:3 Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana awezaye.
5 Kwa kuwa siku zake zimeamriwa, hesabu ya miezi yake unayo wewe,
Nawe umemwekea mipaka yake asiyoweza kuipita;
6 Zab 39:13 Acha kumwangalia yeye, apate kupumzika,
Hata atakapoitimiza siku yake, kama aliyeajiriwa.
7 Kwani yako matumaini ya mti, ya kuwa ukikatwa utachipuka tena,
Wala machipukizi yake hayatakoma.
8 Ijapokuwa mizizi yake huchakaa mchangani,
Na shina lake kufa katika udongo;
9 Lakini kwa harufu ya maji utachipuka,
Na kutoa matawi kama mche.
10 Lakini mwanadamu hufa, hufariki dunia;
Naam, mwanadamu hukata roho, naye yupo wapi?
11 Kama vile maji kupwa katika bahari,
Na mto kupunguka na kukatika;
12 Zab 102:26;Isa 51:6;Mdo 3:21;Rum 8:20;2 Pet 3:7;Ufu 20:14 Ndivyo mwanadamu hulala chini, asiinuke;
Hata wakati wa mbingu kutokuwako tena, hawataamka,
Wala kuamshwa usingizini.
13 Laiti ungenificha kuzimuni,
Ukanilinda kwa siri, hata ghadhabu zako zitakapopita,
Na kuniandikia muda ulioamriwa, na kunikumbuka!
14 Ayu 13:15;Zab 16:10;1 Kor 15:42-58;Flp 3:21 Mtu akifa, je! Atakuwa hai tena?
Mimi ningengoja siku zote za huduma yangu,
Hadi kufunguliwa kwangu kunifikie.
15 Ayu 13:22;Zab 50:4;Yn 5:28;1 The 4:16 Wewe ungeita, nami ningekujibu;
Ungekuwa na tamaa ya kazi ya mikono yako.
16 Kum 32:34;Ayu 10:6,14;13:27;Zab 56:8;Mit 5:21;Yer 32:19;Hos 13:12 Lakini sasa wazihesabu hatua zangu;
Je! Huchungulii dhambi yangu?
17 Kosa langu limetiwa mhuri mfukoni,
Nawe waufunga uovu wangu.
18 Lakini, tazama, mlima ukianguka hutoweka,
Nalo jabali huondolewa mahali pake;
19 Maji mengi huyapunguza mawe;
Mafuriko yake huuchukua mchanga wa nchi;
Nawe matumaini ya wanadamu wayaangamiza.
20 Wewe wamshinda nguvu sikuzote, naye hupita aende zake
Wabadili sura zake, na kumtuma aende mbali.
21 1 Sam 4:20;Zab 39:6;Mhu 9:5;Isa 63:16 Wanawe hufikia heshima, wala yeye hajui;
Kisha wao huaibishwa, lakini yeye hana habari zao.
22 Zab 49:14;Mit 14:32;Mt 8:12 Huhisi tu maumivu ya mwili wake,
Na huombolezea nafsi yake tu.