1 Ndipo huyo Elifazi, Mtemani, akajibu na kusema,
2 Mtu akijaribu kuzungumza nawe, je! Utaona ni vibaya?
Lakini ni nani awezaye kujizuia asinene?
3 Tazama, wewe umewafunza watu wengi,
Nawe umeitia nguvu mikono iliyokuwa minyonge.
4 Maneno yako yamemtegemeza huyo aliyekuwa anaanguka,
Nawe umeyaimarisha magoti manyonge.
5 Mit 24:10;Lk 4:23 Lakini sasa haya yamekufikia wewe, nawe wafa moyo;
Yamekugusa, nawe wafadhaika.
6 Ayu 1:1;Mit 3:26 Je! Dini yako siyo tegemeo lako?
Na matumaini yako si huo uelekevu wa njia zako?
7 Kumbuka, tafadhali, ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia?
Au ni wapi hao waelekevu walikatiliwa mbali?
8 Zab 7:14 Kama mimi nilivyoona, hao walimao maovu,
Na kupanda madhara, huvuna yayo hayo.
9 Kwa pumzi za Mungu huangamia.
Na kwa kuvuma kwa hasira zake humalizika.
10 Ayu 29:17;Zab 3:7 Kunguruma kwake simba, na sauti ya simba mkali,
Na meno ya simba wachanga, yamevunjika.
11 Zab 34:10 Simba mzee huangamia kwa kukosa mawindo,
Nao watoto wa simba jike wametawanyika mbalimbali.
12 Basi, nililetewa neno kwa siri,
Sikio langu likasikia manong’ono yake.
13 Ayu 33:15 Katika mawazo yaliyotoka katika maono ya usiku,
Hapo usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu.
14 Hofu iliniangukia na kutetemeka,
Iliyoitetemesha mifupa yangu yote.
15 Zab 104:4;Mt 14:26;Ebr 1:14 Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu;
Na nywele za mwili wangu zilisimama.
16 Hiyo pepo ilisimama kimya, nisiweze kutambua sura zake,
Mfano ulikuwa mbele ya macho yangu;
Kulikuwa kimya, nami nilisikia sauti, ikinena,
17 Je! Binadamu atakuwa na haki kuliko Mungu?
Je! Mtu atakuwa safi kuliko Muumba wake?
18 2 Pet 2:4 Tazama, yeye hawategemei watumishi wake;
Na malaika wake huwahesabia kosa;
19 Je! Si zaidi sana hao wakaao katika nyumba za udongo,
Ambazo misingi yao i katika mchanga,
Hao wanaopondwa kama nondo!
20 Kati ya asubuhi na jioni huvunjwa-vunjwa;
Waangamia milele wala hapana atiaye moyoni.
21 Je! Kamba ya hema yao haikung’olewa ndani yao?
Nao hufa hata bila kuwa na hekima.