Publicidade

Salmos 14

Uovu Wa Wanadamu
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 Mpumbavu anasema moyoni mwake,

"Hakuna Mungu."

Wameharibika, matendo yao ni maovu kabisa;

hakuna hata mmoja atendaye mema.

2 Bwana anawachungulia wanadamu chini

kutoka mbinguni

aone kama wako wenye akili,

wowote wanaomtafuta Mungu.

3 Wote wamepotoka,

wameharibika wote pamoja,

hakuna atendaye mema.

Naam, hakuna hata mmoja!

4 Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza:

wale ambao huwala watu wangu

kama watu walavyo mkate,

hao ambao hawamwiti Bwana?

5 Wako hapo, wameingiwa na hofu kuu,

maana Mungu yupo pamoja na wenye haki.

6 Ninyi watenda mabaya mnakwamisha mipango ya maskini,

bali Bwana ndiye kimbilio lao.

7 Laiti wokovu wa Israeli

ungalikuja kutoka Sayuni!

Wakati Bwana arejeshapo

wafungwa wa watu wake,

Yakobo na ashangilie,

Israeli na afurahi!

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_06-50-08-