Publicidade

Salmos 62

Mungu Kimbilio La Pekee
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi.

1 Kwa Mungu peke yake nafsi yangu inapata pumziko;

wokovu wangu watoka kwake.

2 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;

yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe.

3 Mtamshambulia mtu hata lini?

Je, ninyi nyote mtamtupa chini,

ukuta huu ulioinama na uzio huu unaotikisika?

4 Walikusudia kikamilifu kumwangusha

toka mahali pake pa fahari;

wanafurahia uongo.

Kwa vinywa vyao hubariki,

lakini ndani ya mioyo yao hulaani.

5 Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake,

tumaini langu latoka kwake.

6 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu;

ndiye ngome yangu, sitatikisika.

7 Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu,

ndiye mwamba wangu wenye nguvu

na kimbilio langu.

8 Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote,

miminieni mioyo yenu kwake,

kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu.

9 Binadamu wa ngazi ya chini ni pumzi tu,

nao wa ngazi ya juu ni uongo tu;

wakipimwa kwenye mizani, si chochote;

wote kwa pamoja ni pumzi tu.

10 Usitumainie vya udhalimu

wala usijivune kwa vitu vya wizi;

ingawa utajiri wako utaongezeka,

usiviwekee moyo wako.

11 Jambo moja Mungu amelisema,

mambo mawili nimeyasikia:

kwamba, Ee Mungu,

wewe una nguvu,

12 na kwamba, Ee Bwana,

wewe ni mwenye upendo.

Hakika utampa kila mtu thawabu

kwa kadiri ya alivyotenda.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-15_21-32-39-