Publicidade

Salmos 21

Shukrani Kwa Mungu Kwa Ajili Ya Ushindi
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 Ee Bwana, mfalme huzifurahia nguvu zako.

Tazama jinsi ilivyo kuu furaha yake

kwa ushindi unaompa!

2 Umempa haja ya moyo wake

na hukumzuilia maombi ya midomo yake.

3 Ulimkaribisha kwa baraka tele

na kumvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.

4 Alikuomba maisha, nawe ukampa,

wingi wa siku milele na milele.

5 Kutokana na ushindi uliompa, utukufu wake ni mkubwa,

umeweka juu yake fahari na utukufu.

6 Hakika umempa baraka za milele,

umemfanya awe na furaha

kwa shangwe ya uwepo wako.

7 Kwa kuwa mfalme anamtumaini Bwana;

kwa upendo usiokoma wa Aliye Juu Sana hatatikiswa.

8 Mkono wako utawashika adui zako wote,

mkono wako wa kuume utawakamata adui zako.

9 Wakati utakapojitokeza

utawafanya kama tanuru ya moto.

Katika ghadhabu yake Bwana atawameza,

moto wake utawateketeza.

10 Utawaangamiza wazao wao kutoka duniani,

uzao wao kutoka wanadamu.

11 Ingawa watapanga mabaya dhidi yako

na kutunga hila, hawawezi kufanikiwa,

12 kwa kuwa utawafanya wakimbie

utakapowalenga usoni pao

kwa mshale kutoka kwenye upinde wako.

13 Ee Bwana, utukuzwe katika nguvu zako,

tutaimba na kusifu nguvu zako.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_06-50-08-