1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya;
mwimbieni Bwana dunia yote.
2 Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake;
tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
3 Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa,
matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
4 Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;
yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,
lakini Bwana aliziumba mbingu.
6 Fahari na enzi viko mbele yake;
nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
7 Mpeni Bwana, enyi jamaa za mataifa,
mpeni Bwana utukufu na nguvu.
8 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake;
leteni sadaka na mje katika nyua zake.
9 Mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake;
dunia yote na itetemeke mbele zake.