Publicidade

Salmos 64

Kuomba ulinzi dhidi ya adui
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1 Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu,

uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui.

2 Unifiche kutokana na njama za waovu,

kutokana na fitina za kundi la watenda maovu.

3 Wananoa ndimi zao kama panga

na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha.

4 Hurusha mishale kutoka mavizio kwa mtu asiye na hatia,

humrushia ghafula bila woga.

5 Kila mmoja humtia moyo mwenzake

katika mipango mibaya;

huzungumza kuhusu kuficha mitego yao,

nao husema, "Ni nani ataiona?"

6 Hupanga njama la dhuluma na kusema,

"Tumebuni mpango mkamilifu!"

Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.

7 Bali Mungu atawapiga kwa mishale,

nao ghafula wataangushwa.

8 Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao

na kuwaleta kwenye maangamizi;

wote wawaonao watatikisa vichwa vyao

kwa dharau.

9 Wanadamu wote wataogopa,

watatangaza kazi za Mungu

na kutafakari yale aliyoyatenda.

10 Wenye haki na wafurahi katika Mwenyezi Mungu,

na wakimbilie kwake;

wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_06-50-08-