Publicidade

Salmos 35

Kuomba msaada: Kuokolewa kutokana na adui
Zaburi ya Daudi.

1 Ee Mwenyezi Mungu, pingana na wale wanaopingana nami,

upigane na hao wanaopigana nami.

2 Chukua ngao na kigao.

Inuka unisaidie.

3 Inua mkuki wako na fumo lako

dhidi ya hao wanaonifuatia.

Iambie nafsi yangu,

"Mimi ni wokovu wako."

4 Wafedheheshwe na waaibishwe

wale wanaotafuta uhai wangu.

Wanaofanya shauri kuniangamiza

wafukuzwe mbali kwa bumbuazi.

5 Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo,

malaika wa Mwenyezi Mungu akiwafukuza.

6 Njia yao na iwe giza na ya utelezi,

malaika wa Mwenyezi Mungu akiwafuatilia.

7 Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu,

na bila sababu wamenichimbia shimo,

8 maafa na yawapate ghafula:

wavu walionifichia na uwatege wenyewe,

na waanguke katika shimo hilo,

kwa maangamizi yao.

9 Ndipo nafsi yangu itashangilia katika Mwenyezi Mungu

na kuufurahia wokovu wake.

10 Nitapaza sauti yangu nikisema,

"Ni nani aliye kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu?

Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale waliowazidi nguvu,

unawaokoa maskini na wahitaji kutokana na wanaowanyang’anya!"

11 Mashahidi wakatili wanainuka,

wananiuliza mambo nisiyoyajua.

12 Wananilipa baya kwa jema

na kuiacha nafsi yangu ukiwa.

13 Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa gunia

na nikajinyenyekeza kwa kufunga.

Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa,

14 niliendelea kuomboleza

kama vile wao ni rafiki au ndugu.

Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni

kama ninayemwombolezea mama yangu.

15 Lakini nilipojikwaa,

walikusanyika kwa shangwe;

washambuliaji walijikusanya dhidi yangu

bila mimi kujua.

Walinisingizia pasipo kukoma.

16 Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki,

wamenisagia meno.

17 Ee Bwana, utatazama hadi lini?

Niokoe maisha yangu na maangamizi yao,

okoa uhai wangu wa thamani

kutokana na simba hawa.

18 Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa,

nitakusifu katikati ya watu wengi.

19 Usiwaache wale wanaonisimanga,

wale ambao ni adui zangu bila sababu;

usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu

wakonyeze jicho kwa hila.

20 Hawazungumzi kwa amani,

bali wanatunga mashtaka ya uongo

dhidi ya wale wanaoishi

kwa utulivu katika nchi.

21 Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, "Aha! Aha!

Kwa macho yetu wenyewe tumeliona."

22 Ee Mwenyezi Mungu, umeona hili, usiwe kimya.

Usiwe mbali nami, Ee Bwana.

23 Amka, inuka unitetee!

Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu.

24 Nihukumu kwa haki yako, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu,

sawasawa na haki yako;

usiwaache wakusimange.

25 Usiwaache wafikiri, "Aha, hili ndilo tulilotaka!"

Au waseme, "Tumemmeza."

26 Wote wanaofurahia dhiki yangu

waaibishwe na wachanganyikiwe;

hao wanaojiinua dhidi yangu

wavikwe aibu na dharau.

27 Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki

wapige kelele za shangwe na furaha;

hebu waseme siku zote, "Mwenyezi Mungu atukuzwe,

ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake."

28 Ulimi wangu utanena haki yako

na sifa zako mchana kutwa.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-15_21-32-39-