Publicidade

Salmos 7

Sala ya mtu anayedhulumiwa
Ombolezo la Daudi kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya Kushi, Mbenyamini.

1 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, ninakukimbilia wewe,

uniokoe na kunikomboa na wote wanaonifuatia,

2 la sivyo watanirarua kama simba

na kunichana vipande vipande, asiwepo wa kuniokoa.

3 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, kama nimetenda haya

na kuna hatia mikononi mwangu,

4 au ikiwa nimemtenda uovu aliye na amani nami,

au nimemnyang’anya adui yangu pasipo sababu,

5 basi adui anifuatie na kunipata,

auponde uhai wangu ardhini

na kunilaza mavumbini.

6 Amka kwa hasira yako, Ee Mwenyezi Mungu,

inuka dhidi ya ghadhabu ya adui zangu.

Amka, Mungu wangu, uamue haki.

7 Kusanyiko la watu na likuzunguke.

Watawale kutoka juu.

8 Mwenyezi Mungu na awahukumu makabila ya watu.

Nihukumu Ee Mwenyezi Mungu,

kwa kadiri ya haki yangu,

kwa kadiri ya uadilifu wangu,

Ewe Uliye Juu Sana.

9 Ee Mungu mwenye haki,

uchunguzaye mawazo na mioyo,

komesha ghasia za waovu

na ufanye wenye haki waishi kwa amani.

10 Ngao yangu ni Mungu Aliye Juu Sana,

anayewaokoa wanyofu wa moyo.

11 Mungu ni mwamuzi mwenye haki,

Mungu anayeghadhibika kila siku.

12 Mtu asipotubu,

Mungu ataunoa upanga wake,

ataupinda na kuufunga uzi upinde wake.

13 Ameandaa silaha zake kali,

ameweka tayari mishale yake ya moto.

14 Yeye aliye na mimba ya uovu

na anayechukua mimba ya ghasia huzaa uongo.

15 Yeye anayechimba shimo na kulifukua

hutumbukia katika shimo alilochimba mwenyewe.

16 Ghasia anazozianzisha humrudia mwenyewe,

ukatili wake humrudia kichwani.

17 Nitamshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili ya haki yake,

na nitaliimbia sifa jina la Mwenyezi Mungu Aliye Juu Sana.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-16_18-40-07-