Pular para o conteúdo
Publicidade

Zaburi 141

Maombi ya kuhifadhiwa dhidi ya uovu

Zaburi ya Daudi.

1 Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita, njoo kwangu hima.

Sikia sauti yangu ninapokuita.

2 Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba;

kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni.

3 Ee Mwenyezi Mungu, weka mlinzi kinywani mwangu,

weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.

4 Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya,

nisije nikashiriki katika matendo maovu

pamoja na watu watendao mabaya,

wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.

5 Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma;

na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu.

Kichwa changu hakitalikataa.

Hata hivyo, maombi yangu daima

ni kinyume cha watenda maovu.

6 Watawala wao watatupwa chini

kutoka majabali,

waovu watajifunza kwamba maneno yangu

yalikuwa kweli.

7 Watasema, "Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi,

ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi."

8 Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi,

ndani yako nimekimbilia, usiniache nife.

9 Niepushe na mitego waliyonitegea,

kutokana na mitego iliyotegwa na watenda maovu.

10 Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe,

wakati mimi ninapita salama.

Veja também