Publicidade

Salmos 107

KITABU CHA TANO

Shukrani kwa kukombolewa katika dhiki

1 Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema,

Kwa maana fadhili zake ni za milele.

2 Na waseme hivi waliokombolewa na BWANA,

Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi.

3 Akawakusanya kutoka nchi zote,

Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.

4 Walitangatanga jangwani katika njia ya nyika;

Hawakuona mji wa kukaa.

5 Waliona njaa na kiu,

Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao.

6 Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,

Akawaponya na shida zao.

7 Akawaongoza kwa njia ya kunyoka,

Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa.

8 Na wamshukuru BWANA, kwa fadhili zake,

Na maajabu yake kwa wanadamu.

9 Maana hushibisha nafsi yenye shauku,

Na nafsi yenye njaa huijaza mema.

10 Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti,

Wamefungwa katika taabu na minyororo,

11 Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu,

Wakalidharau shauri lake Aliye Juu.

12 Hata akawadhili moyo kwa taabu,

Wakajikwaa, wala pasiwe na wa kuwasaidia.

13 Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,

Akawaponya kutoka kwa shida zao.

14 Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti,

Akaivunja minyororo yao.

15 Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake,

Na maajabu yake kwa wanadamu.

16 Maana ameivunja milango ya shaba,

Ameyakata mapingo ya chuma.

17 Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao,

Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa.

18 Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula,

Wameyakaribia malango ya mauti.

19 Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,

Akawaponya kutoka kwa shida zao.

20 Hulituma neno lake, huwaponya,

Huwatoa katika maangamizo yao.

21 Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake,

Na maajabu yake kwa wanadamu.

22 Na wamtolee dhabihu za kushukuru,

Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba.

23 Washukao baharini katika merikebu,

Wafanyao kazi yao katika maji mengi,

24 Hao huziona kazi za BWANA,

Na maajabu yake vilindini.

25 Maana alisema, akavumisha upepo wa dhoruba,

Ukayainua juu mawimbi ya bahari.

26 Walirushwa juu mbinguni, waliteremka hadi vilindini,

Uhodari wao ukayeyuka katika maafa yao.

27 Waliyumbayumba, walipepesuka kama mlevi,

Ujuzi wao wote uliwaishia.

28 Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,

Akawaponya kutoka kwa shida zao.

29 Huituliza dhoruba, ikawa shwari,

Mawimbi yake yakanyamaza.

30 Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia

Naye akawaleta mpaka bandani waliyoitamani.

31 Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake,

Na maajabu yake kwa wanadamu.

32 Na wamtukuze katika kusanyiko la watu,

Na wamhimidi katika baraza la wazee.

33 Amegeuza mito ikawa jangwa,

Na chemchemi za maji zikawa nchi kavu.

34 Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi,

Kwa sababu ya uovu wa wakazi wake.

35 Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji,

Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji.

36 Maana amewakalisha huko wenye njaa,

Nao wamejenga mji wa kukaa.

37 Wakapanda mbegu katika mashamba,

Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake.

38 Naye aliwabariki wakaongezeka sana,

Wala hawapunguzi mifugo wao.

39 Walipopungua na kudhilika,

Kwa kuonewa na dhiki na huzuni.

40 Aliwamwagia wakuu dharau,

Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia.

41 Lakini alimwinua mhitaji juu mbali na mateso,

Na kuwaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo.

42 Wanyofu wa moyo wanaona na kufurahi,

Na waovu wote wananyamazishwa.

43 Aliye na hekima na ayaangalie hayo;

Na wazitafakari fadhili za BWANA.

Veja também

Publicidade
Bíblia Online Bíblia Online

Bíblia Online • Versão: 2026-06-15_21-32-39-