1 Heri amkumbukaye mnyonge;
BWANA atamwokoa siku ya taabu.
2 BWANA atamlinda na kumhifadhi hai,
Naye atafanikiwa katika nchi;
Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake.
3 BWANA atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani.
Katika ugonjwa wake unamponya maradhi yake yote.
4 Nami nilisema, BWANA, unifadhili,
Uniponye roho yangu maana nimekutenda dhambi.
5 Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya,
Atakufa lini, jina lake lipotee?
6 Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo,
Moyo wake hujikusanyia maovu,
Naye atokapo nje huyanena.
7 Wote wanaonichukia wananong'onezana juu yangu,
Wananiwazia yaliyo mabaya zaidi.
8 Wanafikiri pigo liualo limemshika,
Akalala asiweze kusimama tena.
9 Hata rafiki yangu mwandani niliyemtumaini,
Aliyekula pamoja nami,
Ameniinulia kisigino chake.
10 Lakini Wewe, BWANA, unifadhili,
Uniinue nipate kuwalipa.
11 Kwa neno hili nimejua ya kuwa wapendezwa nami,
Kwa kuwa adui yangu hajivunii kunishinda.
12 Nami katika ukamilifu wangu umenitegemeza,
Umeniweka mbele za uso wako milele.
13 Na atukuzwe BWANA, Mungu wa Israeli,
Tangu milele hata milele. Amina na Amina.
KITABU CHA PILI